POLISI BUSEGA WAFANYA USAFI KUTUNZA MAZINGIRA, WAWAKUMBUKA WENYE UHITAJI.

 


Na Mwandishi wetu.

MKUU wa Polisi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Mrakibu wa Polisi (SP) Peter Msafiri, amewaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali katika zoezi la usafi lililofanyika katika Mwalo wa Kabita, wilayani Busega.

Zoezi hilo lililofanyika Agosti 22, 2026, lililenga kuhamasisha wananchi kutunza mazingira, hususan katika maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria, pamoja na kuendeleza ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kulinda mazingira na usalama wa wananchi.



Akizungumza baada ya zoezi hilo, SP Msafiri amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na wahalifu, hasa vinavyotokea katika maeneo ya Ziwa Victoria.

Ninawasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na wahalifu kwa wakati. Taarifa ikitolewa mapema, inasaidia Jeshi la Polisi kuchukua hatua kwa haraka na kuzuia madhara zaidi,” amesema SP Msafiri.


Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kuwa walinzi wa mazingira kwa kuhakikisha taka hazitupwi hovyo katika maeneo ya fukwe na mwalo, akieleza kuwa mazingira safi ni sehemu ya usalama na ustawi wa jamii.


“Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu kwa jamii yetu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunalitunza kwa kuepuka uchafuzi wa mazingira na kushirikiana katika kulinda maeneo haya,” amesisitiza.


Baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi, Jeshi la Polisi Wilaya ya Busega liliendelea na shughuli za kijamii kwa kufanya mjitoleo kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Maega, kilichopo wilayani Busega.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi za kushirikiana na jamii, kuonyesha upendo, mshikamano na kuwajali wananchi wenye mahitaji mbalimbali.


Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, SP Msafiri amesema Jeshi la Polisi linatambua kuwa jukumu lake si kulinda usalama pekee, bali pia kujenga uhusiano mzuri na jamii kupitia shughuli zinazogusa maisha ya wananchi.

Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii. Tunapowafikia watoto na wananchi wenye mahitaji maalum, tunadhihirisha upendo, mshikamano na wajibu wetu wa kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali,” amesema.


Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Polisi na wananchi ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye amani, usalama na mshikamano.

Shughuli hizo zimefanyika ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Polisi Jamii, yanayolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kujenga jamii salama.


Kwa ujumla, shughuli hizo zimeonesha nafasi ya Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa wananchi, kutunza mazingira na kushiriki katika shughuli za kijamii zenye manufaa kwa jamii.

Tunawaomba wananchi waendelee kuwa sehemu ya Polisi Jamii kwa kutoa taarifa, kushirikiana na askari na kushiriki katika shughuli za maendeleo na usalama wa maeneo yao. Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu,” amesema SP Msafiri.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments