MAGANYA ARIDHISHWA NA MRADI WA TACTICS MJINI BARIADI, ATOA MAELEKEZO MAHUSUSI. ‎

‎Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

‎MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya ameridhishwa na ujenzi wa Mradi wa Uboreshaji miji Tanzania (TACTICS) unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bil. 26.5 katika Mji wa Bariadi huku akisisitiza Mradi huo kujengwa kwa ubora na viwango.

‎Mradi huo wa Tactics unatekelezwa katika Mji wa Bariadi utahusisha shughuli za ujenzi wa soko Kuu la Bariadi, Ujenzi wa Ofisi yenye maabara ya Kisasa ya upimaji wa vifaa vya ujenzi na ujenzi wa Barabara za lami katikati ya Mji wa Bariadi.

‎


‎Maganya amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakisha anaweka jicho kwenye Mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati pia ujengwe kwa kuzingatia viwango na ubora.

‎"Mhandisi wa Halmashauri uwe anafika na kuweka jicho lako hapa...mliyosema yafanyike ndani ya muda, msijiche Kwa kichaka cha mvua, pia Chama Cha Mapinduzi, nawaelekeza chezeni nazo na pia wafanyabiashara walikuwepo walikuwa wanafanya Biashara hapa, wako wapi na je, mmewazingatia?" amesema Maganya.

‎


‎Mwenyekiti huyo amewasisitiza Wakandarasi wanaotekeleza Mradi huo kuhakikisha Barabara zinazotengenezwa ziendelezwe ili zitumike na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi huku akiwasisitiza Wahandisi kutojificha kwenye kisingizio cha mvua ili Mradi ikamilika kwa wakati.

‎"Msijenge Barabara halafu hamziendelezi, ujenzi wa Barabara unasababisha kero mbalimbali kwa wananchi, kama mkandarasi hajawa tayari, njia zitumike, hii ni miradi ya CCM, Dk. Samia amepanga kuwaletea maendeleo wananchi kama hizi soko na Barabara, tengenezeni mitaro ya dharura, ili mvua isiathiri Barabara na pia vifusi hasambazwe tuonyeshe Maji yanakopita" amesema.

‎


‎Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Mradi huo, Mratibu wa Mradi huo, Mhandisi Hussein Katakweba amesema Ujenzi wa Mradi huo umefikia asilimia 48, lakini mkandarasi yuko nyuma ya muda kwa asilimia 14 na kwamba unatarajiwa kukamilika mwezi February 2027.

‎Amesema kuwa ujenzi wa Soko pekee unagharimu kiasi cha shilingi Bil. 7, Barabara 13 na Jengo la wahandisi ni shilingi bil. 19.5 ambapo Jumla ya mradi wote ni shilingi Bil. 26.5 na kwamba Mradi ukikamilika utaboresha miundombinu na Uchumi na soko litakuwa na Maduka ya Kisasa.

‎Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga amesema kuwa ujenzi wa soko hilo umezingatia orodha ya wafanyabiashara walikuwepo kwenye soko hilo kupitia namba zao za NIDA pamoja na  majina yao ili ujenzi ukimalika waweze kukabidhiwa vibanda

‎Mwisho.

‎






‎

‎

Post a Comment

0 Comments