DK. ASHREY: MWANAMKE SHUJAA MASWA, ALIYEBADILISHA HUDUMA ZA AFYA KUPITIA BARIKIWA HEALTH CENTER.

Mkurugenzi wa kituo cha Afya BARIKIWA, Dk Ashrey Lucas .

Na Samwel Mwanga, Maswa.

KATIKA wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, kuna hadithi ya mafanikio ya mwanamke mmoja ambaye ameonyesha kuwa dhamira, taaluma na moyo wa kuwahudumia wengine vinaweza kubadilisha maisha ya watu wengi. 

Mwanamke huyo ni Dk. Ashrey Lucas, mkurugenzi wa Barikiwa Health Center, kituo cha afya cha kisasa kilichopo mjini Maswa ambacho kimekuwa tegemeo kwa wananchi wanaohitaji huduma bora za afya.

Kupitia kituo hicho, Dk. Ashrey amefanikiwa kusogeza karibu na wananchi huduma ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana zaidi katika hospitali kubwa za mijini.

Naibu Waziri wa Afya,Dk Florence Samizi(wa kwanza kulia)akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali na wafanyakazi wa kituo cha Afya BARIKIWA baada ya kuweka jiwe la msingi la miaka 10 ya kituo hicho.

Kituo chenye huduma za kisasa.

Barikiwa Health Center kimejipambanua kwa kuwa na vifaa tiba vya kisasa pamoja na wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali. 

Ndani ya kituo hicho, wagonjwa wanapata huduma nyingi muhimu ikiwemo upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za mama na mtoto, afya ya kinywa na meno, pamoja na vipimo vya kisasa vya X-Ray vinavyofanyika katika chumba maalumu cha mionzi.

 


Mbali na hilo, kituo hicho kina wodi zenye mazingira mazuri kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa, huku huduma za uangalizi zikitolewa na wauguzi na madaktari waliobobea.

Jambo lingine linalokipa uzito kituo hicho ni ushirikiano wake na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili,Mloganzila ya jijini Dar es Salaam, ambao hufika Maswa mara kwa mara kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kibingwa. 

Akizungumza kuhusu wazo la kuanzisha kituo hicho, Dk. Ashrey Lucas, ambaye pia Mzaliwa wa wilaya hiyo ni mbobezi wa magonjwa ya kinywa na meno, anasema alisukumwa na hamu ya kuona wananchi wanapata huduma bora karibu yao.

 

Watumishi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha Afya BARIKIWA (wenye mavazi ya kijani)wakitoa maelezo ya jinsi vifaa vya chumba hicho vinavyofanya kazi.

“Niliona wananchi wengi wanapata changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya hasa matibabu ya kibingwa. Hivyo nilitamani kuanzisha kituo kitakachosaidia kupunguza adha hiyo,” anasema.

Wananchi wanavyoona huduma.

Uwepo wa Barikiwa Health Center umeanza kuonekana kama faraja kwa wananchi wengi wa Maswa na maeneo ya jirani.

Mkazi wa Maswa, Jamal Mutende anasema kituo hicho kimepunguza sana changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya matibabu.

 

Watumishi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha Afya BARIKIWA wakitoa maelezo ya jinsi vifaa vya chumba hicho vinavyofanya kazi.

“Zamani tukihitaji vipimo maalumu au matibabu fulani tulikuwa tunakwenda Mwanza au Dar Es Salaam. Lakini sasa huduma nyingi tunazipata hapa hapa Maswa,” anasema.

Naye Eliza Jisephat, mkazi mwingine wa eneo hilo, anasema huduma zinazotolewa zimekuwa zikiwapa wananchi imani kubwa kwa vituo vya afya vya binafsi na jambo moja zuri unatibiwa hata ukiwa na Bima yako ya Afya.

“Huduma ni nzuri na wataalamu wanatupa maelezo ya kina kuhusu afya zetu. Hii inatusaidia kuelewa vizuri matatizo yetu na jinsi ya kujitunza,” anasema.

Wataalamu wa afya wazungumzia mchango wake.

 Kwa upande wa wataalamu wa afya, uwepo wa kituo hicho unaonekana kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya katika wilaya ya Maswa.


Dk. Erick Lumumba ambaye ni mmoja wa wataalamu wanaoshirikiana na kituo hicho, anasema ushirikiano kati ya vituo vya afya binafsi na hospitali kubwa ni muhimu katika kuboresha huduma kwa wananchi.

 “Ushirikiano huu unasaidia kuleta huduma za kibingwa karibu na wananchi badala ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali kubwa,” anasema.

 

Uongozi wa BARIKIWA Heath Center wakitoa misaada mbalimbali kwa mahabusu na wafungwa katika gereza la Maswa.

Serikali yatambua mchango wake.

Viongozi wa serikali pia wamekuwa wakitambua mchango wa kituo hicho katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

 Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akiwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Afya,Mohamed Mchengerwa katika sherehe za miaka 10 ya kituo hicho alisema kuwa uwekezaji wa sekta binafsi katika afya unasaidia kupunguza mzigo katika hospitali za serikali.

 


“Nimpongeze Mkurugenzi wa Kituo cha Afya BARIKIWA kwa uwekezaji huu mkubwa na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na serikali inatambua mchango wa wawekezaji kama hawa kwa sababu wanaongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” anasema.

Kurudisha kwa jamii.

Mbali na kutoa huduma za afya, Barikiwa Health Center imeonyesha pia kujali maendeleo ya jamii. Kituo hicho kimeanzisha timu za mpira wa miguu kwa vijana wa kiume na kike, hatua inayolenga kuhamasisha afya njema na kukuza vipaji vya michezo sambamba na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii katika hospitali ya wilaya ya Maswa kwa wagonjwa,Kwa mahabusu na wafungwa katika gereza la Maswa na kutoa chakula kwa kaya ambazo hazina uwezo hasa nyakati za sikukuu maeneo ya vijijini.

 

Uongozi wa BARIKIWA Heath Center  wakitoa misaada mbalimbali kwa mahabusu na wafungwa katika gereza la Maswa.

Kauli mbiu ya kituo hicho ni “Tunarudisha kwa jamii.”

Kwa mujibu wa Dk. Ashrey, mafanikio ya kituo hicho yanapaswa kwenda sambamba na kuwasaidia wananchi wanaowazunguka.

“Tunaamini kuwa mafanikio ya taasisi yoyote lazima yawe na manufaa kwa jamii inayotuzunguka. Ndiyo maana tunashiriki pia katika shughuli za kijamii,” anasema.

 


Mfano wa kuigwa.

Katika kipindi ambacho sekta ya afya nchini bado inahitaji uwekezaji mkubwa zaidi, juhudi za Dk. Ashrey Lucas zinaonyesha namna mtu mmoja mwenye maono anavyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.

Kupitia Barikiwa Health Center,sio tu kwamba huduma bora za afya zimekaribia wananchi wa Maswa, bali pia ajira zimepatikana kwa wataalamu wa afya,sekta mbalimbali na vijana wamepata fursa kupitia michezo.

 Kwa wengi, Dk. Ashrey Lucas ni mfano wa mwanamke shujaa anayethibitisha kuwa uwekezaji katika afya ni uwekezaji katika maisha ya watu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

 Mwisho.





Post a Comment

1 Comments

  1. Ni jambo la fahari sana,,tuendelee kuwapa taarifa Wana maswa na simiyu Kwa ujumla,, uwepo wa hiki kituo Cha afya ,

    ReplyDelete