Na Samwel Mwanga, Maswa.
MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dkt Vicent Naano amewataka wananchi wa kijiji cha Manawa kata ya Sengwa kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao za kila siku huku akisisitiza kuwa eneo hilo liko salama na hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani.
Hofu hiyo imezuka katika eneo hilo la mpaka kati ya wilaya hiyo na wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga kufuatia kuzuka kwa vurugu katika wilaya hiyo jirani na hivyo kudaiwa waliofanya vurugu kukimbilia wilaya ya Maswa na hivyo jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kuanza kuwatafuta na kuzua taharuki katika kijiji hicho.
Dk Naano ametoa kauli hiyo Juni 3,2026 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo kufuatia hofu iliyojitokeza kwa baadhi ya wananchi kuhusu masuala ya kiusalama.
Amesema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imejipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za maendeleo bila wasiwasi wowote.
“Wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida, hakuna uvunjifu wa amani katika eneo letu. Tunachotaka ni ushirikiano wa wananchi kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kutokuwaficha wahalifu wala kuwakumbatia kwani kufanya hivyo kunachochea kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu katika jamii.
“Wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na vyombo vya dola kwa kuwataja wahalifu ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi wilaya ya Maswa (OCD), SSP Samwel Onyango amewataka wananchi kuwa karibu na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mapema kuhusu vitendo vya uhalifu na watu wanaotiliwa shaka.
Sehemu ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Manawa. Picha na Samwel Mwanga.Amesema ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kuimarika.
“Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao, hivyo wananchi wasiogope kutoa taarifa kwani taarifa zao zitafanyiwa kazi kwa siri na umakini mkubwa,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameeleza kuridhishwa na ujio wa viongozi hao wakisema umewapa matumaini na kuondoa hofu iliyokuwa imejitokeza.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Naomi Ngasa amesema wananchi wengi walikuwa na wasiwasi lakini maelezo yaliyotolewa na viongozi hao yamewapa utulivu.
“Tumefarijika kuona viongozi wamefika kuzungumza nasi moja kwa moja, sasa tunaamini hali ni salama,” amesema.
Mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Maswa(OCD),SSP Samwel Onyango akitoa elimu juu ya ulinzi shirikishi katika kijiji cha Manawa wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga.Naye diwani wa kata ya Sengwa,Mohamed Dasse amesema wananchi wako tayari kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu.
“Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu, tukikaa kimya wahalifu wataendelea kutusumbua,” amesema.
Kwa upande wake, Paulo Shija amesema elimu iliyotolewa imewasaidia wananchi kuelewa umuhimu wa kutotoa hifadhi kwa wahalifu.
“Ni kweli wakati mwingine wananchi wanaogopa kutoa taarifa, lakini sasa tumeelezwa vizuri kuwa ushirikiano na polisi ni muhimu kwa maendeleo ya kijiji chetu,” amesema.
Mwisho.






0 Comments