DC SIMALENGA AWAHIMIZA MADIWANI BARIADI MJI KUSHIRIKIANA UKUSANYAJI MAPATO.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga, akiongea kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Na Mwandishi wetu, Bariadi.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kushirikiana na Wataalamu katika zoezi la ukusanyaji wa mapato pamoja na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato ili kuleta Maendeleo katika Halmashauri hiyo.

Ameyabainishwa hayo leo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmahauri hiyo lililoketi leo 14 Agosti 2026 kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kupindi cha robo ya Nne cha Mwaka wa Fedha 2025/26.

Simalenga amewasisitiza Waheshimiwa madiwani pamoja na wakuu wa idara kuweka msisitizo na misingi imara ya usimamizi bora wa ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kuzuia Mianya ya upotevu wa mapato ya ndani kwa maendeleo ya Bariadi na Nchi kwa ujumla 

"Naomba niwasisitize timu ya Menejimenti ya Halmashauri msimamie kwa makini ukusanyaji wa mapato ili tuendelee kushikilia rekodi ya makusanyo ya 2025/2026 ambayo yamevuka lengo hii itasaidia kukamilisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizopangwa". Amesema Mhe. Simalenga.

Awali akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi Nkenyenge Charles, amewapongeza wataalamu wa Halmashauri hiyo kwa jitihada wanazofanya katika ukusanyaji mzuri wa mapato hali iliyopelekea kuvuka lengo la ukisanyaji wa mapato wa Mwaka wa Fedha 2025/26

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Iddi Ndabhona, amesema kuwa amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na baraza hilo na kwamba yeye pamoja na timu ya Menejimenti ya Halmashauri watayatekeleza kwa weledi mkubwa. 

Katika Mkutano huo ambao uliongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Nkenyenge Charles na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi Ndg. Iddi Ndabhona, Waheshimiwa Madiwani , Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, Taasisi mbalimbali na timu ya Wataalamu wa Halmashauri.

Mwisho.
























Post a Comment

0 Comments