WAZEE WANAUME WADAI KUTAMBULIWA.

Dk Christopher Nzela ambaye ni Mshauri wa Rais wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania akiwaonyesha wazee moja ya dawa za kutumia ili kuondoa sumu mwili.Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

CHAMA  cha Wazee Wanaume Tanzania kimewataka wazee kujiunga na chama hicho ili kuunganisha nguvu na kupaza sauti kwa pamoja katika kudai haki na kutatua changamoto zinazowakabili katika jamii.

Akizungumza leo, Agosti 15, 2026, wilayani Maswa mkoani Simiyu na Wazee kutoka wilaya ya Maswa na Meatu, Mshauri wa Rais wa chama hicho, Dk Christopher Nzela, amesema wazee wanaume wamekuwa kundi linalosahaulika katika jamii na hata katika mipango ya Serikali.

Amesema licha ya halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu, wazee wanaume hawajafaidika na utaratibu huo.

“Agenda yetu kubwa kwa sasa, licha ya kutafuta wanachama nchi nzima, ni kuhakikisha tunatambuliwa na Serikali kama makundi mengine. Ndipo tuanze kudai haki zetu, ikiwamo kila mzee kuwa na bima ya afya inayogharamiwa na Serikali,” amesema Dk Nzela.

Picha mbalimbali za baadhi ya wazee wa wilaya ya Maswa na Meatu ambao wamehudhuria kikao cha Chama cha Wazee Wanaume Tanzania wilaya Maswa.Picha na Samwel Mwanga

Amesema wazee wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na umri mkubwa, ikiwamo maradhi yanayohitaji matibabu ya mara kwa mara, huku gharama za huduma za afya zikiwa mzigo kwa wengi wao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha Taifa wa chama hicho, Mchungaji Christopher Simangole, amesema chama kinaandaa mkutano mkuu utakaofanyika Dodoma Agosti 28 hadi 29,2026, ambao pamoja na mambo mengine utajadili namna ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa wazee wanaume nchini.

Simangole, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, amewataka wazee wanaume wa Simiyu kujenga uongozi imara na kuungana ili waweze kufanya maamuzi yatakayolinda maslahi yao.

Picha mbalimbali za baadhi ya wazee wa wilaya ya Maswa na Meatu ambao wamehudhuria kikao cha Chama cha Wazee Wanaume Tanzania wilaya Maswa.Picha na Samwel Mwanga

“Tuwahamasishe na wenzetu wajiunge na chama chetu. Gharama ya fomu ya kujiunga ni Sh10,000 na katiba ni Sh5,000. Nina imani hatuwezi kushindwa, ila tukumbuke umoja ndiyo silaha yetu muhimu ya kupigania maslahi yetu,” amesema.

Sauti za wazee.

Mussa Mashamba kutoka wilaya ya Meatu anasema kuwa kulingana na umri wao kuwa mkubwa lakini wanakosa sauti ya pamoja ya kusemea changamoto zao.

“Tumekuwa tukikabiliwa na changamoto nyingi baada ya kufikia umri huu, lakini mara nyingi tunakosa sehemu ya pamoja ya kuwasilisha matatizo yetu. Tukijiunga na kuwa kitu kimoja, tutakuwa na nguvu ya kuzungumza na Serikali na wadau kuhusu mahitaji yetu.”amesema.

Ngwegwe Duta kutoka wilaya ya Maswa: amesema kuwa ni vizuri na wao watambuliwe na kuthaminiwa katika jamii.

“Tunataka wazee wanaume tutambuliwe na kusikilizwa. Kuna mambo mengi tunahitaji kusaidiwa, hasa afya na maisha ya kila siku. Serikali ikitambua changamoto zetu, itakuwa rahisi kuweka mipango inayotusaidia.”anasema.

Kwa upande wake Masanja Mboi amesema umoja wao ndiyo njia pekee  ya kudai haki zao.

“Umoja wetu ndiyo njia ya kupata nguvu ya kudai haki. Kama kila mmoja ataendelea kukaa kwake na kulalamika peke yake, ni vigumu kusikika. Tunapaswa kuungana na kuwa na sauti moja.”amesema.

Chama hicho kimewataka wazee wanaume katika mikoa mbalimbali nchini kujiunga na kuimarisha uongozi wa chama ili kuongeza nguvu ya kushinikiza kutambuliwa na kupata fursa na huduma zinazolingana na mahitaji yao.

Mwisho.













Post a Comment

0 Comments