UMITASHUMTA WAHITIMISHWA SIMIYU, WANAMICHEZO WATAKIWA KUWA NA NIDHAMU.

 

Afisa Elimu mkoa wa Simiyu, Khalifa Shemahonge (mwenye miwani) akimkabidhi kikombe mmoja wa wanafunzi kutoka halmashauri ya wilaya ya Meatu wakati akifunga mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa. Picha na Samwel Mwanga

Na Samwel Mwanga, Simiyu.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Khalifa Shemahonge amewataka wanamichezo pamoja na walimu watakaoambatana na timu ya mkoa huo kwenye mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA mkoani Iringa kuwa na nidhamu, kujituma na kushirikiana ili kulinda heshima ya mkoa huo.

Shemahonge alitoa kauli hiyo  Juni 1,2026 wakati akifunga mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa wa Simiyu katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Maswa yaliyowakutanisha wanafunzi kutoka halmashauri sita za mkoa huo.

Amesema michezo kwa sasa si burudani pekee bali imekuwa chanzo cha ajira na mafanikio kwa vijana wengi, hivyo wanafunzi wanapaswa kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuzingatia maadili, nidhamu na juhudi katika mafunzo na mashindano.

Afisa Elimu mkoa wa Simiyu, Khalifa Shemahonge akizungumza wakati akifunga mashindano ya UMITASHUMITA ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Wasichana ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.

“Tunawataka wanafunzi pamoja na walimu wao kuwa na ushirikiano mkubwa na kuhakikisha wanalinda heshima ya mkoa wa Simiyu katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Iringa,” amesema.

Aidha, amewaelekeza Maafisa Elimu Msingi wa wilaya pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi katika mkoa huo kuhakikisha ratiba za michezo na sanaa zinazingatiwa mashuleni kwa kuwa ni sehemu muhimu ya taaluma na maendeleo ya mwanafunzi.

Kwa upande wake, Afisa Michezo Mkoa wa Simiyu, Emanuel Athanas alisema jumla ya wanafunzi 719 kutoka halmashauri sita za mkoa huo walishiriki mashindano hayo katika michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, kwaya pamoja na ngoma za asili.

Afisa Michezo mkoa wa Simiyu,Emanuel Athanas akitoa taarifa ya jinsi mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa yalivyoendeshwa.Picha na Samwel Mwanga.

Amesema kuwa wanamichezo 120 katika michezo mbalimbali wamechaguliwa kuuwakilisha mkoa huo katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika mkoani Iringa.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mashindano hayo walieleza kufurahishwa na ushindani uliokuwepo huku wakisema umeongeza uzoefu na kuwapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.

Mwanafunzi wa shule ya msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mathias Emanuel amesema mashindano hayo yamemjengea uwezo mkubwa wa kujiamini na kushirikiana na wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali.

“Tumefurahia kushiriki mashindano haya kwa sababu yametufanya kujifunza nidhamu, ushirikiano na ushindani wa haki,” amesema.


Kwa upande wake, Rukia Elias kutoka halmashauri ya wilaya ya Bariadi amesema anaamini timu ya Simiyu itafanya vizuri katika mashindano ya kitaifa kutokana na maandalizi mazuri waliyopewa.

“Ninaamini tutafanya vizuri Iringa kwa sababu walimu wetu wametuandaa vizuri na sisi tupo tayari kupambana,” amesema.

Naye Martha Joel kutoka Busega amesema michezo imekuwa njia muhimu ya kuibua vipaji vya wanafunzi wengi na kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

“Michezo inaweza kutufikisha mbali na hata kutupatia ajira baadaye, hivyo tunaomba iendelee kupewa kipaumbele mashuleni,” amesema.

Mwisho.











Post a Comment

0 Comments