SKAUTI WAHIMIZWA KULINDA AMANI, UZALENDO NA KUDUMISHA UMOJA WA KITAIFA.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed (katikati) alipata maelezo namna vijana wa Skauti walivyoshiriki Kambi la kitaaluma lililofanyika St. Aloyce Gonzaga wilayani Maswa.

Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.

VIJANA wa Skauti nchini, Wametakiwa kuendelea kujifunza Uzalendo ili kudumisha Amani ya Tanzania kwa lengo la  kuwa na Umoja wa Kitaifa huku wakisisitizwa kutojiunga kwenye magenge ya Uhalifu yanayochochea uvunjifu wa Amani.

‎Aidha, Wazazi na Walezi wametakiwa kuwaruhusu watoto wao kujiunga na Chama cha Skauti ili vijana wafundishwe Uzalendo, Utu, Amani, Umoja Mshikamano pamoja na kutoruhusu Maovu.

‎Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed wakati akifunga Kambi ya Skauti iliyofanyika Shule ya Seminari St. Aloyce Gonzaga Maswa ambapo aliwasisitiza vijana kulinda Tunu za Taifa, Kudumisha Amani na kulinda Nchi ya Tanzania.

‎Shemsa amewataka Vijana hao kuwa mabalozi wa uzalendo huku akiwasisitiza kwenda kufundisha uzalendo kwa vijana wengine ili waendelee kudumisha amani na Upendo uliopo katika nchi ya Tanzania.

‎"Kafundisheni ndugu zenu maana ya utu na uzalendo, tunatakiwa tuendelee kudumisha Amani na Upendo tulionao kwenye nchi nchi yetu...natamani Skauti ya Uzalendo, ambayo Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Mlezi wa Skauti kitaifa anaitaka, ukijifunza uzalendo hakutakiwa na moyo wa kuichoma moto nchi yako ndio yako, wenye nchi ni nyinyi, msipolinda nchi, ikichomeka hatuna pa kwenda na nchi ni moja tu inaitwa Tanznaia" Amesema Mwenyekiti huyo na kuongeza.

‎"Tuna Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mlezi wenu, tuendelee kudumisha amani ya nchi yetu na kupitia Skauti tunajifunza Uzalendo, Ukakamavu, Utu, Ujamaa...tunataka kuona mnarejesha Skauti ya zamani nami nimekubali kuwachangia kiasi cha shilingi Mil. 1.38 kwa ajili ya Ununuzi wa Sare."

‎Awali, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Simiyu, Mkaguzi wa Polisi, Francis Msuku amemhakikishia Mwenyekiti huyo kuwa watalea Chama Cha Skauti kwa kufuata Misingi, Haki na Uadilifu na kwamba Skauti Mkoa wa Simiyu imekuwa sehemu ya mfano ndani ya Tanzania na kwamba wamepatiwa vyeti vya Utambuzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Simiyu, Mkaguzi wa Polisi, Francis Msuku akizungumza kwenye hafla ya kufunga Kambi la Kitaaluma lililofanyika St. Aloyce Gonzaga wilayani Maswa.

‎Naye Mratibu wa Makambi hayo Mkoa wa Simiyu, Mwalimu Cladus Rwezaula kutoka Nyalikungu Shule ya Msingi amesema Kambi hiyo imehusisha Maskauti 280 kutoka wilaya tano za Mkoa wa Simiyu ambapo Wanawake 88 na wanaume 192.

‎Ameeleza kuwa kupitia kambi za kielemu, vijana hao wamefundishwa uzalendo, Nidhamu, Ukakamavu, Kilimo na utunzaji wa Mazingira.

Pawa Sayi, ambaye ni Skauti kutoka Meatu, amesema kupitia makambi hayo watajifunza uzalendo wa maisha pamoja na kufundishwa mbinu mbalimbali za kutatua changamoto katika maisha yao ya kila siku.

‎Naye Lusia Seni, Skauti kutoka wilaya ya Maswa, amesema kuwa kambi hiyo itawasaidia vijana kuwa wazoefu na kuwa wabunifu, huku akiwataka wazazi kutozuia watoto kupelekwa Skauti.

Mwisho.


















Post a Comment

0 Comments