Na Mwandishi wetu, Bariadi.
KATIKA jitihada za kuendelea Kulinda na Kutetea haki za mtoto nchini, Asasi za Kiraia zimeombwa kuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya malezi bora kuanzia kwa wazazi na walezi ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja juu ya matendo yanayohatarisha usalama wa mtoto.
Rai hilo limetolewa leo tarehe 16 Juni, 2026 na Diwani wa Kata ya Sima, Zebedayo Kingi Diwani katika kilele Cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Sima 'A' huku akiwasisitiza watoto kuwa mstari wa mbele kupinga na kujiepusha na matendo ya kikatili dhidi yao.
"Elimu hizi zisiishie kwa watoto peke yao bali mjikite pia kutoa elimu kwa wazazi na walezi kwani itawasaidia watoto hawa kuwa na uhuru kuanzia ngazi za familia". amesema Zebedayo.
"Aidha ametoa wito kwa wataalamu wa Halmashauri kitengo cha Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatoa elimu kwa makundi yanayochukua mikopo ya asilimia 10 kuacha mazoea ya kuwapa watoto wao biashara na kuwasababishia kukosa haki zao ya msingi ya kupata elimu". Ameongezea Zebedayo.
Akisoma risala mbele ya mgeni Rasmi, Prisca Simba mwanafunzi wa kidato Cha pili shule ya sekondari Simiyu amesema kuwa mbali na maboresho yanayofanyika kumlinda mtoto zipo changamoto zinazowakabiri ikiwa ni pamoja na adhabu kali zisizofaa, ndoa za utotoni, matumizi ya dawa za kulevya na kuiomba jamii mzima kushirikiana kutokomeza vitendo hivyo.
Akitumia maadhimisho hayo hayo Mkaguzi kata ya Gambosi na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Simiyu, Inspekta Francis Msuku ametoa elimu ya ukatili dhidi ya watoto na namna ya kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sehemu husika.
Maadhimisho hayo ya Mtoto wa Afrika yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa" yameadhimishwa ngazi ya Halmashauri katika viwanja vya Shule ya Msingi Sima 'A'.
Mwisho.











0 Comments