
Na Mwandishi wetu, Giriku.
WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Simiyu, na mikoa jirani jana walifurika katika mchezo wa Utamaduni wa kabila la Wasukuma almaarufu Mbina, sherehe ambayo husherehekewa wakati wa mavuno ukihusisha ushindani wa pande mbili za Wagalu na Wagika.
Katika mchezo huo ambao huhusisha mashindano ya kucheza mbina kwa kutumia Dawa, Ngoma, Mabinda, Zeze na maigizo mbalimbali, umekuwa ukikonga nyoyo za mashabiki hali inayoleta furaha, amani Umoja na mshikamano na baada ya michezo hiyo, jamii hukutana pamoja kula ushindi yaani Butambi.
Jana, Mei 21, 2026, Wilaya ya Bariadi imeshuhudia tukio kubwa na la kuvutia la utamaduni baada ya Maelfu ya wananchi kujitokeza kushiriki na kushuhudia ngoma ya asili maarufu kama Mbina, iliyofanyika katika Mtaa wa Giriku, Kata ya Bunamhala, mbina ambayo kufanyika tarehe kama hiyo kila mwaka.
Tukio hilo la kipekee limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bariadi, OCD Jeronime Simon.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Simalenga aliungana na wananchi katika kushiriki burudani hiyo ya kitamaduni, hatua inayoonesha kuthamini na kuendeleza urithi wa mila na desturi za jamii ya eneo hilo. Uwepo wake pamoja na viongozi wengine umeongeza chachu ya hamasa na mshikamano miongoni mwa wananchi waliohudhuria.
Ngoma ya Mbina imeendelea kuwa kivutio kikubwa cha kila mwaka, ambapo pamoja na burudani yake, pia huwakutanisha wananchi katika hali ya umoja, mshikamano na kujivunia utamaduni wao wa asili.
Mbali na tukio kuu, shughuli nyingine ndogo ndogo za kitamaduni hufanyika katika kata zote za Wilaya ya Bariadi, zikiwa na lengo la kuenzi na kuendeleza ngoma za asili pamoja na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Wananchi wamepongeza juhudi hizo zinazoendelea kuhuisha utamaduni, wakisisitiza kuwa matukio kama haya ni muhimu katika kulinda historia, maadili na mshikamano wa jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mchezo huo pia umekuwa kivutio kwa wageni kutoka mikoa jirani ambao hawajawai kuona utamaduni huo unaohusisha matumizi ya dawa za asili, wakati huo vijana wenye umri mdogo wakitumbuiza kwenye majukwaa hayo.
Mwisho.
0 Comments