Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Bayer Tanzania,Mwinyi Sango akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika kijiji cha Giriku mkoani Simiyu jinsi wanavyozalisha mbegu bora za mahindi kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga, Bariadi.

KAMPUNI ya BAYER TANZANIA imeeleza kuwa inaendelea kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu bora za mahindi ili kuwasaidia wakulima kuongeza tija, kupata mavuno mengi na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi. 

Kampuni hiyo imejikita katika kuzalisha mbegu zinazolenga kuongeza usalama wa chakula kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Moja ya sehemu ya shamba darasa la.mahindi lililolimwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo katika kijiji cha Giriku mkoa wa Simiyi linalosimamiwa na kampuni ya Bayer Tanzania. Picha na Samwel Mwanga.

Akizungumza Mei 21, 2026 katika kijiji cha Giriku, halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, wakati wa sherehe za wakulima za kusherehekea mavuno zilizopambwa na ngoma za asili za Kisukuma maarufu kama Mbina, Mkurugenzi Mtendaji wa Bayer Tanzania, Mwinyi Sango, amesema kampuni hiyo inalenga kumwezesha mkulima kufanya kilimo chenye tija kupitia matumizi ya mbegu bora.

Amesema kampuni hiyo huzalisha mbegu za mahindi aina ya DEKALB maarufu kama DKC, ambazo huandaliwa kulingana na mazingira na hali ya hewa ya maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Bayer Tanzania, Mwinyi Sango akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika kijiji cha Giriku mkoani Simiyu jinsi wanavyozalisha mbegu bora za mahindi kwa ajili ya kilimo cha zao hilo. Picha na Samwel Mwanga.

“Sisi leo tupo hapa kusherehekea na wakulima wetu baada ya mavuno. Tunaamini kuwa kilimo bora kinaanza na mbegu bora. Tunajitahidi kuhakikisha mkulima anapata mafanikio kupitia mbegu zetu, lakini pia maafisa ugani wetu kwa kushirikiana na maafisa wa serikali wanaendelea kuwa karibu na wakulima ili kuhakikisha wanalima kilimo cha mahindi kwa tija,” amesema.

Amesema jambo la msingi katika mbegu hizo ni ubora wake pamoja na uwezo wa kuota kwa uhakika, hali inayomwezesha mkulima kupata mavuno makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Mtafiti wa Bayer Tanzania, Maduka Joseph, amesema matumizi ya mbegu zilizoboreshwa ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza uzalishaji wa mahindi na kuhakikisha taifa linakuwa na uhakika wa chakula.

“Tunazalisha mbegu zinazoendana na mazingira yaliyobadilika. Zipo zinazokomaa mapema na nyingine zinazostahimili ukame, hivyo mkulima akifuata kanuni za kilimo anaweza kupata mavuno makubwa zaidi,” amesema.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, baadhi ya mbegu zilizoboreshwa zina uwezo wa kustahimili ukame, magonjwa pamoja na kutoa mavuno makubwa kwa hekta, hatua inayotajwa kuwa suluhisho kwa wakulima wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. 

Wakati kampuni za mbegu zikiendelea kuzalisha aina mbalimbali za mbegu, wakulima wa mkoa wa Simiyu wamezitaka taasisi za utafiti, kampuni za mbegu na wadau wa kilimo kuongeza upatikanaji wa mbegu zinazostahimili ukame ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.

Magasha Malimi, mkulima wa mahindi kutoka kijiji cha Majahida wilayani Bariadi, amesema hali ya hewa imebadilika na kufanya kilimo kuwa na changamoto kubwa kuliko ilivyokuwa awali.

“Hali ya hewa imebadilika sana. Zamani mvua zilikuwa zinajulikana lakini sasa hazitabiriki. Tunahitaji mbegu bora zinazowahi kukomaa na zinazohimili ukame ili tusipate hasara kila msimu,” amesema.

Mkulima Magasha Malimi wa kijiji cha Majahida wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika kijiji cha Giriku jinsi anavyojishugjulisha na kilimo cha mahindi.Picha na Samwel Mwanga.

Naye Neema Daud kutoka kijiji cha Lugulu wilayani Itilima alisema gharama za uzalishaji zimeongezeka, hivyo wakulima wanahitaji mbegu zenye uwezo wa kuongeza mavuno hata katika maeneo madogo.

“Tunatumia fedha nyingi kulima lakini wakati mwingine tunavuna kidogo kutokana na ukame. Tukipata mbegu bora tunaweza kuvuna zaidi hata kwa hekari chache,” amesema.

Kwa upande wake, Shitebo Jiganga kutoka kijiji cha Malita wilayani Maswa amesema pamoja na uwepo wa mbegu bora, bado changamoto ya upatikanaji wake na gharama kubwa vijijini inaendelea kuwa kikwazo kwa baadhi ya wakulima.

Amesema ili kilimo kiwe na tija zaidi, ni muhimu mbegu bora zipatikane kwa urahisi na kwa gharama zinazomwezesha mkulima wa kawaida kuzimudu.

Wadau wa kilimo wanaamini kuwa uwekezaji katika mbegu bora unaweza kuwa hatua muhimu ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuifanya Simiyu kuwa miongoni mwa maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mahindi nchini.

Mwisho.