WALINZI BINAFSI MBARONI KWA KUIBA GARI LA OFISI YA RC SIMIYU.

Gari aina ya Landcruser Hardtop (Kwa hisani ya Mtandao.)

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

‎JESHI la Polisi Mkoani Simiyu linawashikiliwa watu watatu ambao ni walinzi wa Kampuni binafsi (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kuiba gari ambalo ni Mali ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

‎Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Mei 29, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe Imeeleza kuwa, Mei 21, 2026, watuhumiwa watatu waliokuwa walinzi wa kampuni binafsi walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa gari aina ya Landcruiser Hardtop nyeupe yenye namba STM 6285 mali ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.


‎Adha, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, katika kipindi cha Mei 1 hadi Mei 28, 2026, jumla ya watuhumiwa 85 wanaodaiwa kuhusika na makosa mbalimbali ya jinai walikamatwa.

‎Kati ya hao, watuhumiwa 60 wamefikishwa mahakamani na watuhumiwa 35 wamehukumiwa kutokana na makosa yao na katika operesheni hizo, watuhumiwa watano walikamatwa wakiwa na nyara za serikali bila kibali.

‎Nyara hizo ni, Nyama ya pori aina ya punda milia kilo 750, Nyama ya nyumbu kilo 505, Vipande vinne vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 16.

Aidha, jumla ya kilo 140 za dawa za kulevya zilikamatwa, zikiwemo: Mirungi kilo 50 (watuhumiwa 4), Bhangi kilo 90 (watuhumiwa 5), Pia, Mei 28, 2026 polisi waliteketeza shamba la bhangi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja katika Kijiji cha Buhungukila, Wilaya ya Maswa, na kuwakamata watuhumiwa watatu.

‎Katika hatua nyingine, lita 120 za pombe haramu ya gongo zilikamatwa na watuhumiwa watano wanaodaiwa kujihusisha na utengenezaji na usambazaji wake.

‎Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu ametoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na uhalifu, huku akisisitiza kuwa operesheni zinaendelea. Pia amewahimiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu.

‎Mwisho.




Post a Comment

0 Comments