Na Samwel Mwanga, Maswa
JESHI la Polisi wilaya ya Maswa mkoani Simiyu linawashikilia Ndoma Jilala (65), Benjamin Ndoma (28) na Maiko Jilumba (22), wote wakazi wa kijiji cha Buhungukila wilayani humo kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha bangi katika shamba lenye ukubwa wa ekari moja.
Akizungumza na Mei 28, 2026 katika kijiji hicho, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP)Chacha Maro amesema watuhumiwa hao walipanda bangi kwa kuchanganya na mazao mengine ili shughuli hiyo isigundulike kirahisi.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu Chacha Maro akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi walivyowakamata watuhumiwa wa kilimo cha bangi katika kijiji cha Buhungukila wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.Amesema tukio hilo limebainika Mei 28, 2026 kufuatia operesheni maalumu ya kupambana na dawa za kulevya iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliotoa taarifa za siri kuhusu uwepo wa shamba hilo.
Kwa mujibu wa Maro, miche hiyo ya bangi ilikuwa imepandwa kwa ustadi mkubwa katikati ya mimea ya pamba kwa lengo la kuficha shughuli hiyo haramu.
“Ukamataji huu ni mwendelezo wa mkakati thabiti na endelevu wa Jeshi la Polisi katika kuthibiti na kutokomeza kilimo cha bangi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya. Tutapita katika kona zote za mkoa wetu wa Simiyu kuhakikisha tunakomesha kilimo hiki,” amesema.
Amesema baada ya kuikata miche hiyo ambayo mingi ilikuwa imekomaa, polisi waliinteketeza kwa kuichoma moto huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na shughuli hizo haramu kwa kuwa bangi ni kichocheo cha uhalifu katika jamii.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu, Chacha Maro (mwenye barakoa) akiangalia jinsi mimea ya bangi inavyoteketezwa katika kijiji cha Buhungukila wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi tumeteketeza miche yote ya bangi huku taratibu nyingine za kisheria zinaendelea kufuatwa,” amesema.
Polisi wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu ikiwemo kilimo na usafirishaji wa dawa za kulevya ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Wananchi wakishirikiana na askari polisi wakikata miche ya bangi katika shamba lililopo katika kijiji cha Buhungukila wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Buhungukila wamesema operesheni hiyo imekuwa funzo kwa watu wanaojihusisha na shughuli haramu wakiamini kuwa hawatagundulika.
Doto Jimola mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa ushirikiano kati ya wananchi na polisi umeonesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
“Ni vizuri watu wakaacha kulima bangi kwa sababu inaleta madhara makubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla,” amesema.
Watuhumiwa watatu waliokamatwa na jeshi la polisi wilaya ya Maswa ambayo wanadaiwa kulima zao la bangi katika kijiji cha Buhungukila.Picha na Samwel Mwanga.
Daud Ntemi amesema uwepo wa mashamba ya bangi katika eneo hilo ulikuwa ukichangia kuharibika kwa maadili ya vijana pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.
“Wapo vijana ambao tayari walikuwa wanaanza kuharibika kitabia kutokana na matumizi ya bangi. Tunaomba operesheni hizi ziendelee mara kwa mara,” amesema.
Naye Bahati Seni ambaye ni mkulima katika kijiji hicho amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mashamba ya mazao ya biashara kama pamba kuficha kilimo cha bangi jambo ambalo linapaswa kukemewa na jamii nzima.
“Kilimo halali kinatosha kutupatia kipato. Hakuna sababu ya kuingia katika mambo haramu ambayo mwisho wake ni matatizo na kuvunja amani ya kijiji,” amesema.
Mwisho.








0 Comments