VIFAA TIBA VYA MIL. 20 VYAKABIDHIWA SIMIYU KUPAMBANA NA UKIMWI.


Na Mwandishi wetu.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la AIDS HEALTHCARE FOUNDATION (AHF) limekabidhi Serikali ya Mkoa wa Simiyu vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI na kuboresha huduma za afya katika vituo mbalimbali vya afya.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo mei 13, 2026 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu iliyopo Nyaumata, Wilaya ya Bariadi, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anamringi Macha amepokea vifaa hivyo na baadaye kuvikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga kwa ajili ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Bariadi pamoja na Zahanati ya Dutwa.

AHF imeendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kupambana na UKIMWI kupitia utoaji wa vifaa tiba, elimu ya afya na uhamasishaji wa jamii kuhusu kujikinga na maambukizi ya VVU, hatua ambayo inalenga kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika vituo vya afya.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Macha amelishukuru shirika hilo kwa mchango wake mkubwa na ametoa wito kwa jamii hususani vijana kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi mapya ya VVU.

Msaada huu unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments