MAAFISA MAENDELEO YA JAMII BUSEGA WAKABIDHIWA PIKIPIKI KUONGEZA UWAJIBIKAJI.



Na Mwandishi wetu.

MAAFISA Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wamekabidhiwa pikipiki kila mmoja,  ikiwa ni vitendea kazi vitakavyowawezesha kuongeza ufanisi wa kazi kwa kuwafikia wananchi hususani walioko vijijini kwa wakati kwa ajili ya kuwahudumia.

Akikabidhi pikipiki hizo katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Faidha Salimu amewataka maafisa hao kwenda kutumia vitendea kazi hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha amewasistiza kuwafikia wananchi vijijini na kuwaelimisha kuhusu fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali bila riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Wenyeulemavu ili waweze kuunda vikundi na kuomba mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi ya ujasiriamali, na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Katika hatua nyingine amewataka kwenda kuwaelimisha wananchi kujiepusha na mikopo umiza maarufu kausha damu, badala yake wakope kwenye taasisi za kifedha zinazotambulika na serikali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Hamidu Hamisi amesema halmashauri hiyo itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma kwa kutatua changamoto zinazowakabili, huku akiwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwahudumia wananchi ipasavyo, hasa ikizingatiwa kwamba idara hiyo inategemewa na Taifa katika kufikia maendeleo endelevu.

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Busega, Flora Barakana amesema pikipiki hizo zimegharimu shilingi milioni 62, ikiwa ni juhudi za serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Katika kuwezesha makundi ya Wanawake, Vijana na Wenyeulemavu kiuchumi, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Busega, imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 586 kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Machi mwaka wa fedha 2025/2026 kwa makundi hayo.

  Mwisho. 






Post a Comment

0 Comments