Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, limeendelea na Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi na kusisitizwa juu ya Ukusanyaji wa Mapato.
Akizungumza katika Mkutano huo wa Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Nkenyenge Charles amewataka Madiwani pamoja na Viongozi wa Halmashauri kuongeza juhudi na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa Fedha Halmashauri ya Mji wa Bariadi imeweza kukusanya asilimia 89.1 kupitia mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mafanikio hayo yamepatikana ikiwa bado mwezi Mmoja kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, hali inayoonesha kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali za Halmashauri pamoja na ushirikiano mzuri kati ya Viongozi, Watendaji na Wananchi katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka .
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga ametumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato hadi kufikia robo ya tatu hali itakayopelekea kuvuka lengo la asilimia 100 la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Sambamba na hilo Simalenga amemtaka Meneja wa TARURA wilaya ya Bariadi kuhakikisha wanafungua barabara zilizoharibika katika kipindi cha mvua ili kuwawezesha Wananchi wa Bariadi kuendelea na shughuli za kimaendeleo bila kuwa na vikwazo vya barabara.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Iddi Ndabhona ametumia nafasi katika Baraza hilo la Madiwani kutoa zawadi za pesa taslim za pongezi kwa Walimu Wakuu waliofanya vizuri katika usimamizi wa Miradi ya Maendeleo katika Shule pamoja na uongozi bora shuleni .
Mwisho.
![]() |











0 Comments