Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Simon Simalenga, ameendelea na ziara yake katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi huku akiwaonya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ya Serengeti na pori la Akiba la Maswa kitojihusisha na Ujangili.
Ziara hiyo imefanyika katika kata za Matongo, Mwantimba na Masewa ambapo pamoja na mambo mengine wananchi walipata nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ikiwemo ubovu wa Barabara, wananchi kuvamia na wanyama wakali kama Tembo na Simba pamoja na huduma za Afya zisizoridhisha.
Aidha, Katika mkutano uliofanyika kata ya Matongo, wananchi walizungumzia changamoto ya utozwaji wa fedha kwa ajili ya kumuona daktari pamoja na hali mbaya ya baadhi ya barabara zinazohitaji ukarabati wa haraka pamoja na Elimu ya uhifadhi.
Diwani wa Kata ya Matongo, Masunga Keya alisema kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya Maji licha ya Mradi wa Maji kukamilika lakini umekosa wasimamizi ili kuhudumia wananchi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya barabara, Meneja wa TARURA Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hussein Katakweba, amesema tayari serikali imeanza ukarabati wa barabara kuu tatu ikiwemo ya kata ya Matongo.
Ameeleza kuwa barabara ya Nyawa Shuleni – Gilya – Mwauchumu yenye urefu wa kilomita sita tayari imekamilika, huku kazi ya ukarabati katika maeneo ya Mwauchumu na Salalia ikiendelea. Amesema iwapo mitambo haitapata hitilafu, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki hii.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndugu Khalid Mbwana, akatoa elimu kuhusu huduma za afya katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali, hasa kuhusu gharama za kumuona daktari na matibabu kwa watoto pamoja na wajawazito.
Ameeleza kuwa huduma ya kumuona daktari katika zahanati ni bure, huku gharama katika Kituo cha Afya Matongo ikiwa ni shilingi elfu mbili kutokana na sera iliyopo. Aidha, alisema gharama zinaweza kuongezeka kulingana na aina ya huduma au vipimo vinavyohitajika.
Pia amefafanua kuwa huduma za wajawazito ni bure kwa huduma za ujauzito pekee, lakini iwapo mama mjamzito atahitaji matibabu ya magonjwa mengine atalazimika kugharamia huduma hizo.
Afisa Mhifadhi na Kamanda wa pori la Kijereshi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Floravicky Kalambo, amepiga marufuku kwa mwananchi yeyote kumiliki au kukaa na mnyama pori bila kuwa na kibali halali kutoka kwa mamlaka husika.
Amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori au viungo vya mwanyamapori.
Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na serikali pamoja na taasisi za uhifadhi kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uwindaji haramu ili kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Uhifadhi wa wanyamapori unachangia kukuza utalii, kuongeza mapato ya serikali na kuboresha maendeleo ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kijamii".
Katika ujumbe wake kwa Wananchi, Simalenga aliwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kushiriki vikao vya maendeleo na kuwauliza viongozi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Hairuhusiwi kuingiza Mifugo ndani ya hifadhi, mlioanzisha makazi karibu na hifadhi mtoke sababu mkiendeleza makazi pembezoni mwa hifadhi mnajiweka hatari ya maisha yenu...acheni Ujangili sababu haulipi na serikali itawakamata, Rais Dk. Samia ametangaza utalii kupitia wanyama na tunapata fedha za miradi" amesema.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanaofaulu kuingia kidato cha kwanza na kidato cha tano wanapelekwa shule kwa wakati ili kuendelea kupata elimu.
Simalenga pia amezungumzia hatua ya serikali kujenga shule mpya ya msingi pamoja na maandalizi ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Matongo, hatua ambayo itapunguza umbali wa wanafunzi kufuata elimu katika maeneo ya Mwantimba na kata jirani.
Mwisho.

0 Comments