DC MASWA AWAONYA VIONGOZI WA AMCOS WANAOHUJUMU ZAO LA PAMBA.

Mkuu wa wilaya ya Maswa Dkt Vicent Naano akizungumza katika kikao cha viongozi wa Amcos wilayani humo katika ukumbi wa zamani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Na Samwel Mwanga, Maswa.

MKUU wa wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu Dkt. Vicent Naano amewataka wenyeviti wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kusimamia kwa uadilifu makabidhiano ya madawa ya pamba (viuatilifu) kati ya makatibu waliovuliwa nyadhifa zao na wale wapya walioteuliwa, ili kulinda maslahi ya wakulima.

Akizungumza April 30,2026 katika kikao cha viongozi wa AMCOS wilayani humo, amesema kuwa hatua ya kuwaondoa baadhi ya makatibu imelazimika kutokana na tuhuma nzito zinazohusisha ubadhirifu na vitendo vya kuhujumu sekta ya pamba.

Alibainisha kuwa baadhi ya makatibu hao wanadaiwa kuhusika na uharibifu wa mizani ya kielektroniki (mizani janja) iliyokuwa ikitumika katika ununuzi wa zao la pamba msimu wa 2025/2026, hatua iliyochangia kuwaumiza wakulima kwa kupoteza haki zao.

“Tumeshuhudia vitendo vya wizi wa fedha za wakulima, makampuni ya ununuzi qa pamba,ubadhirifu wa mali za vyama, pamoja na upotevu wa viuatilifu na mbegu za pamba. Haya ni makosa makubwa ambayo hayavumiliki,” amesema.

Dkt Naano amesema kuwa pia kumekuwepo na malalamiko dhidi ya baadhi ya makatibu hao wakijihusisha na vitendo vya wizi na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi wa pamba, jambo linalochangia kudhoofisha imani ya wakulima kwa mfumo wa ushirika.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza wenyeviti wa AMCOS kuhakikisha wanasimamia kwa karibu zoezi la makabidhiano ili kuzuia upotevu wa mali na kuhakikisha kila kitu kinahesabiwa na kukabidhiwa kwa uwazi.

“Uadilifu uwe kipaumbele chenu. Hakikisheni hakuna mali ya mkulima inapotea katika kipindi hiki cha mpito. Yeyote atakayebainika kufanya ubadhirifu hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi wapya walioteuliwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ushirika ili kurejesha imani ya wakulima na kuongeza tija katika sekta ya pamba wilayani humo.

Kwa upande wake Afisa Ushirika wilaya ya Maswa, Cosmas Budodi amewataka wenyeviti hao kuzingatia utaratobu wote wa makabidhiano hayo ili kuhakikisha ushirika unamnufaisha mkulima.

"Mkuu wa wilaya hapa ametupatia ujumbe mzuri sana cha kufanya ni kwenda kuyatekekeza na tukifanya hivi ushirika wetu utaaminiwa na wakulima ambao ndiyo msingi wetu mkubwa wa kuwatumikia,'amesena.

Afisa Ushirika wa wilaya ya Maswa,Cosmas Budodi akizungumza katika kikao cha viongozi wa Amcos wilayani humo katika ukumbi wa zamani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Kwa upande wao, baadhi ya wenyeviti wa AMCOS wameahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha uwajibikaji unaimarika na mali zote za vyama zinalindwa kwa manufaa ya wanachama na wakulima kwa ujumla.

Luhanga Solomoka ni Mwenyekiti wa Amcos ya Bushitala amekiri kuwepo.kwa wizi unaofanywa na baadhi ya makatibu qa Amcos hivyo ni vizuri wakapewa elimu ili kujiepusha na vitendo hivyo.

"Kweli wizi upo unaofanywa na baadhi ya makatibu kwa kuhujumu viuatilifu na wizi qa fedha za wakulima kwa ushauri wangu hawa watendaji wa Amcos wakapewa elimu na aliyekosea apewe onyo ili ajifunze,"amesema.

Joseph Mwala ni Mwenyekiti wa Amcos ya Iyogelo amesema kuwa watendaji wote wa Amcos wanaojihusisha na vitendo vya aina yoyote vya ubadhilifu wa pembejeo za wakulima na wizi wa fedha za wakulima ni vizuri hatua za kisheria dhidi yao vikachukuliwa ili kukomesha tabia hiyo.


Baadhi ya Viongozi wa Amcos wakiwa kwenye mkutano wa Mkuu wa wilaya ya Maswa Dkt Vicent Naano (hayupo pichani).

Naye Mwandu Matanga ambaye ni mwenyekiti wa Amcos ya Masela amesema kuwa si vizuri kulea vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa Amcos ni vizuri wahusika wote wakafikishwa katika vyombo vya sheria na kupatiwa adhabu stahiki kulingana na makosa yao waliyoyafanya.

Hatua hiyo inatarajiwa kuleta nidhamu mpya katika usimamizi wa vyama vya ushirika, huku serikali ikisisitiza kuwa haitamvumilia kiongozi yeyote atakayehujumu juhudi za kuinua uchumi wa wakulima wa pamba.

Mwisho.




Post a Comment

0 Comments