Afisa Maendeleo ya jamii wa Mauwasa,Quen Mlagala (aliyesimama) akielezea manufaa ya mradi wa maji katika vijiji vya Mwasita na Mwabayanda pindi utakapokamilika.Picha na Samwel Mwanga.Na Samwel Mwanga, Maswa.
WANANCHI zaidi ya 12,216 wa vijiji vya Mwabayanda ‘S’ na Mwasita, wilayani Maswa mkoani Simiyu, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 2.1 chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA).
Mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji kwenye mnara wenye urefu wa mita 12, lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji, pamoja na ulazaji wa bomba kwa umbali wa kilomita 17.
Aidha, mradi huo utajumuisha ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji, ambapo kila kijiji kitapata vituo vitano.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwasita wilaya ya Maswa waliohudhuria mkutano wa hadhara juu ya ujenzi wa mradi wa maji.Picha na Samwel Mwanga.Akizungumza Aprili 18, 2026 kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa MAUWASA, Juvenary Paschal, amesema kazi hiyo inatekelezwa na mkandarasi Zhongii Contractor Ltd na inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo husika.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kujiandaa kuvuta huduma ya maji hadi majumbani mwao mara baada ya kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kukamilika Mei 2027, ili kuongeza ufanisi na urahisi wa matumizi ya huduma hiyo.
Mhandisi Juvenary Paschal wa Mauwasa akielezea jinsi mradi wa maji wa vijiji vya Mwasita na Mwabayanda wilaya ya Maswa utakavyotekelezwa.Picha na Samwel Mwanga.Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa MAUWASA, Quen Mlagala, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
“Tutahakikisha upatikanaji wa maji unaongezeka kutoka siku tatu hadi siku saba kwa wiki, ili wananchi wapate huduma ya uhakika,” amesema.
Diwani wa Kata ya Ngwighwa, Stephen Dwese, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo, akieleza kuwa utasaidia kumaliza changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika vijiji hivyo.
Diwani wa Kata ya Nghwigwa wilaya ya Maswa, Stephen Dwese akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwasita juu ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa maji.Picha na Samwel Mwanga.“Mradi huu ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Kwa muda mrefu tumekuwa tukikabiliwa na uhaba wa maji, lakini sasa tuna matumaini ya kupata huduma ya uhakika,” amesema.
Mkazi wa kijiji cha Mwasita, Paulina Petro, amesema mradi huo utarahisisha maisha yao na kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
“Maji yakipatikana kwa urahisi tutapata muda zaidi wa kufanya shughuli za uzalishaji mali, hasa sisi wanawake tunaobeba jukumu la kuyatafuta,” amesema.
Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho, Zacharia Bufumbe, amesema mradi huo utaleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi, ikiwamo kuboresha afya za wananchi na kuongeza muda wa kushiriki shughuli za maendeleo.
MWISHO.



0 Comments