SHULE YA MSINGI MAWANDA YAKARABATIWA KWA NGUVU ZA WANANCHI.

 


Na Mwandishi Wetu, Moshi

WANAFUNZI wapatao 75 katika shule ya msingi Mawanda iliyopo katika kata ya Mwika Kusini wilaya ya Moshi  sasa wameanza kupata elimu yao katika mazingira rafiki zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla ya ukarabati unaoendelea kufanywa shuleni hapo.

Awali, kabla ya kufanyika kwa ukarabati huo uliotokana na nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo, wanafunzi hao hawakuwa na mazingira rafiki ikiwemo baadhi ya kuta za majengo kuwa hatarini kuanguka sambamba na mengine kukosa sakafu.

Kutokana na kadhia hiyo wadau hao walihamua kuikarabati shule hiyo kongwe ili iweze kurudia katika hadhi yake ya kawaida na kuondoa kero zilizokwamisha upatikanaji sahihi wa elimu 


Mwenyekiti wa maendeleo ya kata ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwika Kusini, John Tarimo amesema wadau hao kwa kiasi kikubwa waliona sii vyema kukaa kimya na kuiachia serikali pekee kila jambo wakati lipo chini ya uwezo wao.

"Wameona sii vyema kusubiri serikali kufanya kila kitu wakati kuna mambo mengine ambayo wanayamudu na ndio maana wakahamua kuikarabati shule hii ili iweze kurudia hali yake ya awali" amesema.

Kwa mujibu wa diwani huyo ni kuwa bado ipo miradi kadhaa inayoendelea kutekelezwa katika kata hiyo kwa nguvu za wananchi na kuwa bado milango ipo wazi kwa ambao wapo tayari katika kusogeza gurudumu la maendeleo mbele zaidi


'Kwa kuwa lengo ni kuleta maendeleo basi niseme tu milango ipo wazi kwa ambao wana nia ya kutuunga mkono katika kuleta maendeleo katika kata yetu hii' amesema.

Tarimo amesema kuwa ipo haja sasa kwa wananchi kubadili mitizamo kuwa kila kitu kitafanywa na serikali na badala yake waamini kuwa wao ndio sehemu ya mabadiliko hayo wanayoyataka.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiruweni Kati kijiji cha Kiruweni Jackson Machang'u amesema bado michango inahitajika na kuwa suala la maendeleo sio la mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wachache bali kila mwananchi anapaswa kuwajibika katika hilo.

Mwisho. 



Post a Comment

0 Comments