Na Mwandishi Wetu, Moshi
FEDHEHA iliyokuwa ikiwakabili walimu sita wa shule ya msingi Karoro iliyopo kata ya Mwika Kusini wilaya ya Moshi kwa kujisaidia choo kimoja na wanafunzi sasa inaenda kutamatika baada ya wananchi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga choo cha kisasa cha walimu hao.
Walimu hao walikuwa wakipishana na wanafunzi katika choo kimoja na wengine kuamua kutumia vyoo vya majirani hali iliyowapelekea fedheha wakati wakihitaji huduma hiyo muhimu.
Tayari wananchi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo katika kata hiyo wameanza ujenzi wa choo cha walimu hao ambapo kukamilika kwake kutaenda kuondoa adha waliyokuwa wakiipata hapo awali.
Bariki John mkazi wa Karoro anasema kukamilika kwa choo hicho ni jambo la furaha ambalo litaenda kuleta staha kwa walimu hao na kuwa bado nguvu za kiuchumi zinahitajika ili kumalizia kazi iliyobaki.
'Kazi inaenda vizuri tunashukuru kwa kila aliyejitolea ila bado hatujamaliza na tunatakiwa kuhakikisha hii kazi inaenda kumalizia kwa wakati ili tuendelee na miradi mingine ya kimaendeleo' anasema.
Happy Mlay anasema ni jambo la kujivunia kuona kuwa wananchi wakihamua kufanya jambo la maendeleo inawezekana badala ya kusubiria wahisani hata kwa vitu kidogo kama choo.
'Ingekuwa aibu kusubiri ufadhili wa choo wakati sisi wenyewe tunaweza kukijenga hii inatia hamasa wakati serikali ikiwaza mambo makubwa sisi haya madogo ni vyema tukayamaliza sisi wenyewe'anasema.
John Tarimo ni diwani wa kata ya Mwika Kusini wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo anasema wananchi kwa sasa wana mwamko mkubwa katika maendeleo na kuwa ipo haja kwa wananchi wakaendelea kuelimishwa juu ya ushiriki wao katika maendeleo.
'Maendeleo ni lazima yachangiwe na kila mtu na hata hapa tulipofika ni jitihada za wananchi hawa niendelee kuwasihi hata wale ambao bado hawajajitokeza waone umuhimu wakufanya hivyo'anasema
Mwisho.

0 Comments