Na Mwandishi Wetu, Moshi.
DIWANI wa Kata ya Mwika Kusini wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, John Tarimo amewataka wakazi wa kata hiyo kutunza miradi mbali mbali ya kimaendeleo inayoendelea kutekelezwa katika kata hiyo kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Miradi hiyo inatajwa kuwa ni chachu ya maendeleo hivyo kuendelea kuitunza itaenda kufikia malengo yaliyokusudiwa na pia kuwezesha serikali kufanya mambo mengine badala ya kurudia jambo moja kila wakati.
Kwa mujibu wa Tarimo ni kuwa katika kata hiyo ipo miradi kadhaa inayoendelea kutekelezwa kwa nguvu za wananchi kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ambapo hadi sasa baadhi ya miradi ipo kwenye hatua nzuri.
Mradi wa kwanza kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 64 katika kijiji cha Kiruweni ambapo pia wananchi wanatakiwa kufukua mitaro sasa kuhakikisha maji ya mvua zinazoendelea kunyesha hawaathiri barabara hizo.
Kadhalika katika shule ya msingi Karoro ambapo ujenzi wa choo cha walimu unaendelea ili kuondoa adha iliyokuwa ikiwakumba walimu wapatao 6 kujisaidia choo kimoja na wanafunzi mradi huu Bado upo mbioni kukamilika
Pia ukarabati wa ofisi ya walimu uwekaji wa sakafu katika baadhi ya vyumba vya madarasa shule ya msingi Mawanda unaendelea na umefikia hatua nzuri ila bado haujakamilika.
Hata hivyo bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mangi Marialle unaendelea ambapo sasa pindi litakapokamilika huenda kiwango cha ufaulu kwa wasichana kikaongezeka.
Wananchi katika kata hiyo, Anael Shao na Bertha Mlay wamesema kuwa miradi hiyo inatakiwa kulindwa kwa nguvu zote kwani ni michango ya wananchi na kamwe wasiwafumbie macho watu wanaoonekana kutaka kuihujumu.
Mwisho.



0 Comments