WACHIMBAJI WADOGO MWAKITOLYO WAIANGUKIA SERIKALI KUPUNGUZA TOZO KUBWA.

 Wachimbaji wadogo wakijadiliana jambo.


Suzy Butondo, Shinyanga

Wachimbaji wadogo wa madini katika migodi iliyopo kata ya Mwakitolyo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wameiomba serikali kuharakisha maridhiano kuhusu tozo mpya ili waweze kurejea kwenye shughuli zao za uzalishaji, baada ya kusimama kwa takribani wiki mbili.

Wachimbaji hao walitoa ombi hilo hivi karibuni walipozungumza na waandishi wa habari, wakieleza kuwa wamesitisha uchimbaji wakipinga tozo ya shilingi 200,000 kwa kila gari linalobeba mawe kutoka mgodini, wakidai kuwa ni kubwa kupita kiasi.

Mchimbaji mdogo wa Mwakitolyo, Meshack Ngusa, alisema gharama za uendeshaji zimeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufanya shughuli hiyo kukosa tija. Aliongeza kuwa tozo hiyo imewalemea kutokana na kipato kidogo wanachopata, hivyo kuiomba serikali kuipunguza.

Kwa upande wake, Janeth Ngangula alisema wachimbaji wako tayari kulipa tozo, lakini kiwango kilichowekwa ni kikubwa mno. Alisisitiza kuwa kamati iliyoundwa inapaswa kuharakisha mchakato wa kupitia upya tozo hiyo ili wachimbaji waweze kurejea kazini.

“Tunaiomba serikali iharakishe mchakato wa maridhiano. Tozo hii imetuweka katika hali ngumu na tumeshindwa kufanya kazi; tunasubiri suluhisho la haraka kwani hali ni mbaya,” alisema Janeth.

Naye Frank Moshi alipendekeza tozo hiyo ipunguzwe kutoka shilingi 200,000 hadi 20,000 kwa kila gari, akisema kiwango hicho kinaweza kuendana na uhalisia wa uzalishaji na kuwapa wachimbaji nafasi ya kuendelea na kazi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri, alisema kusimama kwa uchimbaji kumeathiri si wachimbaji pekee bali pia shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea sekta hiyo katika eneo hilo.

“Bado hatujapata muafaka wa tozo ya shilingi 200,000 ambayo ni kubwa. Tunaomba ipunguzwe ili tupate faida. Tumesimamisha uzalishaji tangu Machi 31 na hali ni ngumu, lakini tunaendelea kuvumilia tukisubiri maridhiano,” alisema Waziri.

Mwishoni mwa Machi mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alikutana na wachimbaji hao kusikiliza malalamiko yao, na kuunda kamati inayojumuisha wachimbaji pamoja na wataalamu kutoka halmashauri ili kupitia upya tozo hiyo na kufikia muafaka.


Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri, akizungumza
















Post a Comment

0 Comments