Baadhi ya wananchi wa mjini Maswa ambao walipata majiko banifu ya kutumia mkaa kidogo kwa gharama nafuu.Picha na Samwel Mwanga.
Samwel Mwanga,Maswa.
HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imepokea majiko banifu 1247 ya kutumia mkaa ikiwa ni suluhisho muhimu la haraka katika kukabiliana na changamoto ya nishati ya kupikia na uharibifu wa mazingira.
Akizungumza April 16,2026,Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa wakati wa mapokezi ya majiko hayo amesema kuwa yatasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kuboresha afya za wananchi.
Majiko hayo yametolewa kupitia mradi wa usambazaji unaotekelezwa na kampuni ya Geita Millennium Star Ltd.
“Majiko haya ni suluhisho la haraka kwa changamoto ya nishati ya kupikia. Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa katika matumizi ya kuni, kupungua kwa ukataji miti holela na kuboreshwa kwa afya za wananchi wetu,” amesema.
Aliongeza kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha majiko hayo yanawafikia walengwa waliokusudiwa, hasa wananchi wa hali ya chini, kwa kuweka mfumo madhubuti wa usambazaji na ufuatiliaji.
![]() |
Amesema kuwa mradi huo unalenga kunufaisha mamia ya kaya wilayani humo kwa kuwawezesha kutumia nishati kwa ufanisi zaidi, kupunguza gharama za upishi na muda unaotumika kutafuta kuni, hasa kwa wanawake na watoto.
"Pamoja na juhudi hizo, bado mahitaji ya majiko hayo ni makubwa ikizingatiwa kuwa wilaya ya Maswa ina takribani wakazi 426,000, wengi wao wakiishi vijijini na kutegemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia,'amesema.
Naye meneja usambazaji wa majiko kutoka kampuni ya Geita Millennium Star Ltd, Khamis Yahaya, amesema gharama halisi ya jiko moja ni Sh 41,000, lakini kutokana na ruzuku ya serikali, wananchi watalipia Sh 5,250 pekee.
Meneja Usambazaji wa Majiko Banifu wa Kampuni ya Geita Millenium Star Ltd, Khamis Yahaya akitoa maelezo kwa wananchi wa wilaya ya Maswa jinsi ya kutumia jiko hilo.Picha na Samwel Mwanga.“Serikali imeamua kugharamia sehemu kubwa ya gharama hizi ili kupunguza uharibifu wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi wa kipato cha chini,” amesema.
Mkazi wa Sola mjini Maswa Maria Nyamongo, amesema majiko hayo yatapunguza muda unaotumika kutafuta kuni na kutoa nafasi kwa wanawake kujihusisha na shughuli nyingine za maendeleo.
“Tunatumia muda mwingi kwenda porini kutafuta kuni. Kama majiko haya yatapunguza matumizi, yatatusaidia sana na hata kutupa muda wa kufanya shughuli nyingine,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Lalago, Juma Chacha, alisema kupanda kwa bei ya mkaa kumekuwa changamoto, hivyo majiko hayo yatasaidia kupunguza gharama za maisha.
“Bei ya mkaa imekuwa juu siku hizi, hivyo jiko linalotumia mkaa kidogo litakuwa nafuu kwetu,” amesema.
Naye Rehema Mohamed, mama lishe mjini Maswa, alisema moshi umekuwa kikwazo katika shughuli zake za upishi.
“Moshi unatuchosha na kuathiri afya. Kama majiko haya yanapunguza moshi, yatatusaidia kufanya kazi katika mazingira bora zaidi,” amesema.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama umeme, gesi na majiko banifu, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa rasilimali za misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwisho.




0 Comments