MADIWANI MASWA WAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BIL. 51.



 Na SAMWEL MWANGA. Maswa.


BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh 51 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wakiahidi kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

 

Akizungumza Februari 16,2026,Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo,Maisha Mtipa amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni elimu,afya,kilimo na viwanda,

 

Amesema bajeti hiyo ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo,ruzuku ya uendeshaji ofisi na mishahara.

 

Bajeti hiyo iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani imeelezwa kulenga kuimarisha sekta za elimu, afya, kilimo na viwanda, ambazo zimekuwa vipaumbele vikuu vya halmashauri hiyo.

 

Akizungumza wakati wa kuwasilisha rasimu hiyo, Afisa Mipango wa halmashauri hiyo,Julius Ikongora alieleza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali kuu pamoja na mahitaji halisi ya wananchi wa Maswa.

 

Mkakati wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa ajili ya  utekelezaji wa mpango wa bajeti hiyo ni pamoja na kuundwa kwa kikosi kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya minada,magulio na vituo vya kuuzia mazao na kusimamia utaratibu wa stakabadhi ghalani ili kurahisisha uuzaji wa mazao.

 

Pia kuhamamisha kilimo cha mazao ya kimkakati ya biashara ya pamba,choroko,alizeti na mpunga na kuendelea na ujenzi wa vibanda 12 vya biashara katika eneo la stendi ya zamamni kwa lengo la kuongeza mapato..

 


Halmashauri imekadria kukusanya sh 51,049,747,000/=kwa mchanganuo kuwa Sh 4,553,509,000/= zinazotokana na mapato ya ndani, sh 34,050,844,000/= ruzuku ya mishahara,Sh1,849,973,000/=ruzuku ya matumizi mengine.

 

Bajeti ya miradi ya maendeleo (Ruzuku) ni sh 10,595,421,000/=ikijumuisha fedha za ndani sh5,632,686,000/= na fedha za nje sh 4,962,735,000/-.

 

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani walichangia mjadala huo wakitaka kuwepo kwa usimamizi madhubuti wa miradi ili kuondoa malalamiko ya ucheleweshaji na ubadhirifu wa fedha za umma, pia walitaka kipaumbele kiwekwe katika miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi vijijini.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Maisha Mtipa alibainisha kuwa sehemu kubwa ya bajeti hiyo inatarajiwa kutoka Serikali Kuu, huku mapato ya ndani yakitarajiwa kuchangia sehemu nyingine. Aliahidi kuwa ofisi yake itasimamia utekelezaji kwa kuzingatia sheria na taratibu za fedha za umma.

 


Kupitishwa kwa rasimu hiyo sasa kunafungua hatua ya maandalizi ya utekelezaji rasmi mara baada ya kupokea idhini kutoka mamlaka husika

 Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments