- DC Naano aagiza mkakati maalum
Na SAMWEL MWANGA,MASWA
WILAYA ya Maswa mkoani Simiyu bado inakabiliwa na upungufu wa madawati 12,606 katika shule za msingi, hali inayowalazimu wanafunzi wengi kukaa chini wakati wa masomo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha bajeti kilichofanyika mjini Maswa, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano, ameitaka halmashauri kuweka mpango mkakati wa haraka kumaliza tatizo hilo.
Amesema hali ya upungufu wa madawati ni mbaya licha ya uwepo wa viongozi katika maeneo mbalimbali, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti.
“Madiwani twendeni katika maeneo yetu tukatatue tatizo la upungufu wa madawati kupitia kamati zetu za maendeleo ya kata. Tukipanga vizuri na kuwaeleza wananchi, tunaweza kulimaliza,” amesema Dkt. Naano.
Ameongeza kuwa atakuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wananchi ili kuhakikisha kila mwanafunzi anasoma akiwa amekaa kwenye dawati, akilitaja suala hilo kuwa agenda ya pamoja kwa wilaya nzima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, kipaumbele katika sekta ya elimu ni utengenezaji wa madawati ili kupunguza na hatimaye kuondoa upungufu uliopo.
‘Katika bajeti yetu ijayo suala la utengenezaji wa madawati tumelipatia kipaumbele na kwa kuanzia tutatengeneza madawati 3252 na kuyasambaza kwewnye shule ambazo zina upungufu mkubwa,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Miza Jishuli, amewataka madiwani kulipa uzito suala hilo na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Kwa mujibu wa takwimu za Halmashauri, mahitaji halisi ya madawati katika shule za msingi wilayani humo ni 34,868, yaliyopo ni 24,263 huku upungufu ukiwa madawati 12,606 sawa na asilimia 48.
Vumia Masanja ni mzazi wa wananfunzi katika shule ya msingi Mlimani wilayani humo amesema kuwa licha ya elimu kutolewa bila malipo lakini kitendo cha wanafunzi kukaa chini hii hali haikubaliki ni vizuri kuhakikisha madawati yanapatikana.
“Mimi kama mzazi ninaona hali hii inaumiza sana. Mtoto anatoka nyumbani asubuhi kwenda shule lakini anakaa chini hadi jioni. Hii inawakatisha tamaa watoto na hata ufaulu unashuka. Tunaomba viongozi wasimamie hili kwa vitendo, nasi tuko tayari kuchangia nguvu kazi.”amesema.
Joyce Paul ni mwanafunzi wa shule ya msingi Matalambuli wilayani humo amesema kuwa inakuwa ni vigumu sana kuandika wananfunzi wakiwa wamebanana katika dawati moja.
“Tunakaa wanafunzi watatu au wanne kwenye dawati moja, wengine chini. Inakuwa vigumu kuandika vizuri. Tunaomba tupatiwe madawati ya kutosha ili tusome kwa amani kama shule nyingine.”amesema.
MWISHO.



0 Comments