Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Serikali imesikia na inatambua Kilio cha wananchi juu ya kupanda kwa Bei ya saruji huku akiwahakikishia wananchi kuwa suala hilo la mfumuko wa Bei ya Saruji linashughulikiwa.
Akizunguma kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya CCM Mjini Bariadi, Dk. Mwigulu amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesikia Kilio cha wananchi na ameelekeza wachukue hatua za haraka ili kidhibiti mfumuko wa bidhaa hiyo muhimu.
"Serikali ya CCM chini ya Rais Samia imesikia Kilio Cha wananchi wake juu ya kupanda kwa bei ya saruji, nimetoa wiki moja ya kufanya tathimini ili tuone namna bora ya kushusha bei ya saruji...serikali inachukua hatua za haraka ili kuhakikisha bei ya saruji inakuwa himilivu ili kila Mtanzania aweze kuhimili kununua saruji hiyo, ndani ya wiki hii uamuzi utakuwa umefanyika ili tuweze kushughulikia tatizo hili na wananchi waendelee kujiletea Maendeleo" amesema.
Amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo kama mikoa ya kusini bei imepanda mpaka kufikia shilingi 26,000, 27000 mpaka 30,000 hivyo wamejipanga kuhakikisha bei inashuka ili kuwa himilivu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepiga Marufuku masuala ya kukamatwa bodaboda na kirikuu badala yake watumike utaratibu wa kufuata Sheria bila kubugudhi wananchi.
Awali Mbunge wa Jimbo wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo ameipongeza serikali kujenga Mradi wa soko la Stendi unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bil. 26.5, Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bil. 440 pamoja na ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme unaotekelezwa kwa shilingi Bil. 56.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge ameipongeza serikali kwa kuboresha sekta za Afya kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu iliyoo Nyaumata, kujenga Shule ya Wasichana ya Simiyu ambayo umelenga kutokomeza ndoa za utotoni
MWISHO.




0 Comments