Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba amewataka Wakandarasi wanaotekeleza Ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme na njia ya kusafirishia Umeme katika Mkoa wa Simiyu, kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili Mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika Kijiji cha Sapiwi wilaya Bariadi ambapo amesema kuwa serikali imeanza kutekeleza mradi wa Gridi Imara katika maeneo saba, na eneo mojawapo ni la Ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme Imalilo katika Mkoa wa Simiyu.
Ameleeza kuwa Utekelezaji wa Mradi huo unalenga kuongeza usambazaji wa Umeme ili kuondoa kukatikakatika Kwa Umeme ambapo serikali imejipanga kuongeza vituo vya kufua Umeme kwani zamani Umeme ulilengwa ufike Makao Makuu ya wilaya, na sasa vijiji vyote vimefikia na Umeme huku ilani ya CCM ikielekeza kufika kwenye vitongoji.
"Niwatake Wakandarasi kituo cha kupozea Umeme na njia ya kusafirishia Umeme, waongeze kasi, wafanye kazi usiku na mchana ili baada ya Mradi huo kukamilika wananchi wafanye kazi ya kujiletea Maendeleo...wafanye kazi usiku na mchana, wanaojenga transmission line na kituo, najua fedha wanayo, kituo cha kupozea umeme wana shilingi Bil. 8, na transmission Wana fedha."
Waziri Mkuu amesema kuwa nchi ya Tanzania imepiga hatua kwenye uzalishaji wa Umeme ambapo hadi Sasa kuna Megawati 2000 za Umeme wa ziada na kwamba kukamilika kwa kituo hicho, Mkoa wa Simiyu utakuwa na Umeme wa uhakika.
Mradi wa kituo cha kupozea Umeme unajengwa kwa gharama ya Shilingi Bil. 8 na pia Mradi wa njia ya kusafirishia Umeme kutoka Ibadakuli mpaka Bariadi wenye urefu wa kilometa 110 unatekelezwa Kwa gharama ya Shilingi Bil. 48.
Mwisho.







0 Comments