Na COSTANTINE MATHIAS, Shinyanga.
WATUMISHI wa Umma wametakiwa kulinda mafao yao kwa kujiepusha na Matapeli huku ikielezwa kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF) hauna mawakala katika hupatikanaji wa mafao.
Hayo yamebainishwa leo na Afisa Msimamizi wa Mfuko huo kutoka Mkoa wa Simiyu, Salum Miraji kwenye mafunzo ya siku moja yaliyofanyika ukumbi wa Karena mjini Shinyanga ambayo yalikutanisha Waandishi wa Habari kutoka Mikoa ya Simiyu na Shinyanga kwa ajili ya kujenga uelewa wa pamoja juu ya Mfuko huo na mafao yake kwa wanachama ambao ni Watumishi wa Umma.
Afisa Msimamizi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Simiyu Salum Miraji Mwegelo akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Amesema kuwa Mfuko huo hauna Mawakala wanaoweza kuwasaidia watumishi wa Umma kupata mafao yao baada ya kustaafu na badala yake huduma zake zinapatika Ofisi za PSSSF kwa kila Mkoa.
"Mfuko una Ofisi kila Mkoa isipokuwa wilaya za Karagwe, Kahama na Korogwe, hatuna Mawakala na huduma zake zinapatikana ofisini, huduma pia zinapatikana Mtandaoni kupitia PSSSF portal na PSSSF kiganjani ambapo mstaafu anaweza kujihakiki" amesema.
Miraji amewataka watumishi wa Umma na Wastaafu kutembelea ofisi za PSSSF kwani kupitia matapeli wanaweza kuwaibia pensheni zao pamoja, msimbo (password) pamoja na kiwacheleweshea kupata pensheni.
Awali akitoa maada kuhusiana na umuhimu wa mafunzo hayo, Mwakilishi wa Meneja wa PSSSF Mkoa wa Shinyanga, Sunday Rashid amesema kazi ya Mfuko huo ni Uandikishaji, kukusanya michango, Uwekezaji pamoja na ulipaji wa mafao kwa wanachama hivyo waandishi wa habari uwa mafunzo hayo yamelenga kuongeza maarifa kwa Waandishi wa habari ili waweze kuripoti taarifa za Mfuko huo kwa usahihi.
Sunday amesema kuwa Mfuko huo una Mafao ya Uzeeni, Ulemavu, kifo, warithi, uzazi, ukosefu wa ajira, na Ugonjwa kwa Watumishi wa Umma.
Mratibu wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Kadama Malunde amewashukuru PSSSF kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamelenga kuongea ujuzi, kukuza maarifa ili waandishi wa habari waweze kuripoti kwa usahihi juu ya mafao ya Watumishi wa Umma.
Malunde amewataka waandishi wa Habari kuzingatia Usahihi wa taarifa, nidhamu na Uwajibikaji katika shughuli zao za kila siku ikizingatia wananchi wanategemea taarifa sahihi kutoka kwa waandishi wa habari wenye weledi.
Mwenyekiti wa Shinyanga Press Club (SPC), Greyson Kakuru amewapongeza PSSSF kwa kunoa ujuzi wa waandishi wa Habari ili waweze kutoa taarifa kwa usahihi ili na jamii iweze kuelezwa kwa usahihi shughuli zinazofanywa na Mfuko huo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Simiyu Press Club (SMPC), Paschal Michael amewataka wanadishi wa habari kutimiza wajibu wao pamoja na kuinua changamoto wanazokumbana nazo watumishi wa Umma ili ziweze kutatuliwa na Mfuko huo.


































0 Comments