Na COSTANTINE MATHIAS.
Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kuongeza uzalishaji na tija ya zao la pamba nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Menejimenti ya Bodi ya Pamba Tanzania na TARI kilichofanyika tarehe 18 Septemba 2026 katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Makao Makuu, Mwanza, ambapo pande hizo zimejadili namna ya kuunganisha utafiti na mahitaji halisi ya wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Mhandisi Godwin Makori, aliipongeza TARI kwa kuendelea kufanya tafiti zinazogusa moja kwa moja uzalishaji wa pamba, ikiwemo afya ya udongo, mbegu, magonjwa ya mimea, mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi ya zana na teknolojia za kilimo.
Mhandisi Makori alisisitiza umuhimu wa matokeo ya utafiti kumfikia mkulima kwa wakati, huku akitoa wito kwa wataalamu wanaohudumia wakulima kuwa na uelewa mpana wa matokeo hayo ili waweze kutoa ushauri unaolenga kutatua changamoto zinazowasilishwa kutoka mashambani.
Alieleza pia umuhimu wa kuimarisha tafiti za mbegu zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kubuni zana rahisi za kukabiliana na changamoto ya magugu, pamoja na kuimarisha ukaguzi wa mbegu katika hatua zote za uzalishaji na usambazaji ili kupunguza kuenea kwa magonjwa ya pamba.
“Moyo wa maendeleo ya nchi ni utafiti, lakini thamani ya utafiti inaonekana pale matokeo yake yanapomfikia mtumiaji wa mwisho na kutatua changamoto aliyonayo,” alisema Mhandisi Makori.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, alisema TARI itaendelea kuimarisha tafiti bunifu zinazozingatia maendeleo ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika kilimo na kutoa suluhisho kwa changamoto za wakulima.
Alisema TARI ina wataalamu zaidi ya 1,400 nchini ambao wako tayari kushirikiana na wadau katika kuendeleza tafiti zenye tija.Dkt. Bwana alieleza kuwa kwa sasa kuna aina 17 za mbegu za pamba zilizo katika hatua mbalimbali za utafiti, na TARI itafanyia kazi pendekezo la Mkurugenzi Mkuu wa TCB kuwa na aina zaidi ya moja za mbegu kwa matumizi ya kibiashara.
Aidha, alieleza kuwa Gene Bank inayojengwa Arusha itasaidia kuhifadhi vinasaba vya mbegu kwa muda mrefu. Katika eneo la teknolojia, Dkt. Bwana alieleza umuhimu wa kuchunguza matumizi ya Akili Unde (AI) katika utambuzi wa magonjwa ya pamba, ikiwemo mnyauko fusari, ili kuwezesha utambuzi na hatua za udhibiti kuchukuliwa mapema.
Viongozi hao pia walisisitiza kuendelea kwa ushirikiano katika kukamilisha mchakato wa usajili wa mbolea hai ya pamba “Go-Biofert”, ili kwenda sambamba na mkakati wa TCB wa usimikaji wa kiwanda cha uzalishaji wa mbolea hiyo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuunda Kamati ya Pamoja ya Wataalamu kutoka TCB na TARI itakayoratibu masuala ya utafiti, ushauri wa kitaalamu na mfumo wa mawasiliano na mrejesho kati ya wakulima, watafiti na wadau, ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafika kwa mkulima na kutumika katika kutatua changamoto za uzalishaji wa pamba.
Mwisho.





0 Comments