Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (mwenye koti la kaki katikati) akikata utepe kuashiria kukabidhi pampu 120 kwa ajili ya shughuli za kilimo cha Umwagiliaji, pampu ambazo zimetolewa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Na COSTANTINE MATHIAS.
SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Kilimo cha Umwagiliaji katika Mkoa wa Simiyu Kwa lengo la kuleta suluhisho kwa wakulima wanaojihusisha na Kilimo cha Umwagiliaji.
Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo, kuongeza uzalishaji na tija, kuhakikisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wakulima, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kufanikisha azma hiyo, Serikali ya awamu ya sita kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ukurasa wa 31, imesisitiza na kuweka mkazo katika kuhakikisha inaongeza maeneo ya kilimo cha umwagiliaji na kuwezesha wakulima na vijana miundombinu na vifaa vya umwagiliaji ili kufikia malengo yao na kuongeza tija kwenye uzalishaji ,kipato na usalama wa chakula.
Hivyo Kupitia ilani ya chama, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kutekeleza Mpango wa Serikali wa kuongeza maeneo ya umwagiliaji kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji na kusambaza pampu za umwagiliaji kwa vikundi vya wakulima, vijana na wanawake ili kufikia malengo ya serikali ya uzalizaji wenye tija, kukuza uchumi na usalama wa chakula Kwa Mkoa wa Simiyu.
Katika Mkoa huo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imekabidhi bure pampu 120 za Umwagiliaji zenye thamani ya shilingi Milioni 864 katika vikundi 120 vinavyojishughulisha na Kilimo cha Umwagiliaji katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (mwenye koti la kaki) akiifanyia majaribio ya kumwwaga Maji pampu iliyotolewa na serikali kwa ajili ya vikundi vya Umwagiliaji Mkoani humo.
Wanufaika wa pampu hizo wanatoka katika Halmashauri za Bariadi Mji wamepata pampu tano (sawa na vikundi vitano), Bariadi vijijini pampu 25 (vikundi 25), Maswa pampu 20 (vikundi 20), Busega pampu 60 (vikundi 60), Itilima pampu 5 (vikundi 5) na Meatu Pampu 5 (vikundi 5).
Ugawaji wa vifaa hivyo unalenga kuongeza tija, kurahisisha kazi za kilimo, kubadilisha mfumo wa kilimo cha kutegemea mvua, na kuongeza kipato cha wakulima wadogo pamoja na kuchangia pato la taifa kwa kutoka kwa wakulima mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Simiyu, Julius Lazaro amesema kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetoa pampu hizo bure kwa Vikundi vya wakulima wanaojihusisha na Kilimo cha Umwagiliaji ili kuwaongezea vipato kupitia shughuli za Kilimo.
Anasema kuwa vikundi hivyo vimekabidhiwa pampu baada ya kukidhi vigezo ikiwemo kuwa na chanzo cha uhakika cha Maji, kuwa na shamba la kufanya Kilimo cha Umwagiliaji na pia chama au kikundi kusajiliwa kwa kutambuliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji baada ya kukidhi vigezo.
"Wakulima wawe na wenye eneo au mashamba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, Kuwepo na chanzo cha maji ya uhakika kama vile Mito, Mabwawa na Ziwa...Wakulima wawe wamejiunga katika umoja wa wakulima wamwagiliaji uliosajiliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Tume ya Taifa ya umwagiliaji" amesema na kuongeza.
"Umoja au kikundi hicho kiwe na uongozi unaotambulika, wenye jukumu la kuratibu shughuli za umwagiliaji, kusimamia matumizi pamoja na kuhakikisha wanachama wote wananufaika kwa usawa na uwekezaji wa Serikali pamoja na kufuata sheria na kanuni zote za Tume ya taifa ya umwagiliaji kwenye usimamizi na uendeshaji wake."
Anaeleza kuwa serikali itaendelea kuboresha na kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo Mabwawa na visima ili kuwezesha wakulima wadogo kulima majira yote ya mwaka, na hivyo kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.
Mhandisi Lazaro anasema kwa Sasa wanatekeleza miradi mikubwa, ya kati na midogo ya Umwagiliaji ikiwemo kujenga Mabwawa kama bwawa la Kasoli ambalo limegarimu zaidi shilingi Bil. 8 na linabeba kata mbili na vijiji zaidi ya vinane ambavyo vitahudumiwa na kutokana na Bwawa hilo.
Anaeleza kuwa kupitia miradi ya kati, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wanajenga mabanio mtoni na kupeleka mifereji kwa wakulima ili waweze kufanya shughuli za kilimo kwa ngazi ya Umwagiliaji pia hawajasahau wakulima wadogowadogo kama hao walioko Mkoa wa Simiyu ambao wamekabidhiwa pampu.
"Maeneo ambayo hayana vyanzo, tunachimba visima ili kuwa na Maji ya uhakika kwa ajili ya shughuli za kilimo ili kuwafikia wananchi wote..Mkoa wa Simiyu tumepanga kuchimba visima 30, ambapo kila Halmashauri tutachimba visima sitasita" anasema.
Kuhusu watu wenye Ulemavu ambao wanaojihusisha na shughuli za kilimo, Mhandisi Julius alisema kuwa hawajapata taarifa na endapo watapatiwa taarifa, kikundi hicho watapewa kipaumbele zaidi kwa sababu ndio kundi kubwa la idadi ya watu ambalo liko mtaani na hawana shughuli za kufanya.
UMILIKI WA PAMPU HIZI.
Anasema kuwa Pampu hizi ni mali ya Serikali na zinakabidhiwa kwa vikundi vya wakulima kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji wenye tija kupitia shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
"vikundi vyote vinawajibika kutunza na kutumia pampu kikamilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa." anasema Mhandisi Lazaro.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Anamringi Macha, anawasihi wanufaika kuzitumia zana hizo kuongeza uzalishai pia kulima kilimo chenye tija.
Macha anawataka wakulima hao kulinda pampu hizo kwa umakini mkubwa ili zilete manufaa endelevu, huku akitoa maelekezo kwa wataalamu wa kilimo mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima na kuwapa elimu stahiki ya kilimo cha kisasa.
"Mmepewa pampu hizi bure na serikali ili mjinufaishe kiuchumi, fanyeni kazi kwa tija ili muweze kunufaika, lengo la serikali ni kuwawezesha ili mjikwamue kiuchumi ninyi wakulima mnaojishughulisha na Kilimo cha Umwagiliaji" anasema Macha.
Juma Kisinza ambaye ni mmoja wa Wanufaika, aliipongeza serikali kwa kutoa pampu hizo ambapo kupitia Kilimo cha Umwagiliaji watajiongezea vipato na kukuza Uchumi wa familia.
UTEKELEZAJI WA MRADI WA PAMPU ZA UMWAGILIAJI SIMIYU.
Kutokana na serikali kugawa pampu hizo, katika Mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wakulima 1,440 waliounganishwa katika vikundi 120, ambapo kati ya hao ni wanawake 576 na wanaume 864.
Kupitia pampu hizi, jumla ya ekari 2400 zinatarajiwa kumwagiliwa, Ambapo litapunguza utegemezi wa kilimo cha mvua na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Hivyo miongoni mwa mazao ynayolimwa ni pamoja na zao la mahindi, ambapo uzalishaji wake unatarajiwa kuongezeka kutoka wastani wa tani 1 kwa ekari hadi kufikia kati ya tani 1.8~ 2.5 kwa ekari.
Aidha, kwa mazao ya bustani hususan nyanya,vitunguu na mazao ya mbogamboga ambapo uzalishaji unatarajiwa kuongezeka kutoka wastani wa tani 6 kwa ekari hadi kufikia tani 10 kwa ekari.
Pampu hizi zimekusudiwa kutumika na vikundi vya wakulima hasa vijana na wanawake waliokidhi vigezo vya uwepo wa vyanzo vya uhakika wa maji kama vile mito, maziwa na mabwawa pia eneo la umwagiliaji.
Vigezo hivyo vimezingatia uwezo wa pampu wa kumwagilia takribani ekari 20 kwa saa moja na kutumia mafuta aina disel lita nne kwa saa.
Pampu hii ina sifa ya kurusha maji kwa kimo cha mita 65, kusukuma maji umbali zaidi ya mita 300m, Kutoa maji 22lita kwa sekunde na Nguvu ya pampu ni 45Hp.
Sambamba na mpango huu, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji kama (ujenzi wa bwawa Kasoli) wenye thamani ya shilingi Bil. 8 na lina uwezo wa kumwagilia eneo lenye ukubwa wa ekari 1875.
Pia kupitia mradi huo wa Bwawa, kutakajengwa miundombinu ya umwagiliaji mashambani yenye thamani ya shilingi Mil. 11 na kunufaisha wakulima zaidi ya 1500.
Aidha, Mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwenye miradi 26 wenye thamani ya shilingi Bil. 1.88 na kuongeza eneo la umwagiliaji 52,500 ekari na kunufaisha wakulima zaidi ya 60,000 pamoja na Ukarabati wa miradi miwili ya Bukangilija na kinamwigulu wenye thamani ya shilingi Bil 1. wenye eneo la ekari 7,500 ekari na kunufaisha wakulima 8000.
Aidha kwa mkoa wa Simiyu eneo la umwagiliaji litaongezeka toka eneo la ekari 5000 hadi kufikia eneo la 63,075 ekari, jumla ya gharama ya miradi yote ya umwagiliaji inayoendelea na kutegemewa kuanza kwenye mkoa wa Simiyu ina thamani ya shilingi Bil 21.9 ambapo miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Aidha Ofisi iko kwenye hatua za mwishoni za mpango wa kuongeza vyanzo vya uhakika vya maji kwa kuchimba visima virefu thelasini kwenye halmashauri zote sita zilizopo mkoa wa Simiyu ili kufanikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongeza eneo la umwagiliaji ekari 1200 ambapo itaongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.
Mwisho.



0 Comments