Na Samwel Mwanga-Simiyu.
KUNA mambo ambayo jamii huyazoea kwa muda mrefu kiasi cha kuacha kujiuliza kama bado yanafaa kuendelea kuwepo.
Adhabu ya viboko shuleni ni miongoni mwa mambo hayo, Kwa miaka mingi, fimbo imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya kawaida ya malezi na ujenzi wa nidhamu kwa wanafunzi.
Hoja imekuwa kwamba mtoto asipopigwa hawezi kuwa na nidhamu na kwamba kizazi cha zamani kilipigwa na kikawa na mafanikio.
Lakini wakati umefika kwa Serikali, wataalamu wa elimu, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kujiuliza swali moja muhimu: Je, mtoto anahitaji kupigwa ili awe na nidhamu?.
Serikali inapaswa kuanza mchakato wa kuondoa kabisa adhabu ya viboko shuleni na kuweka mfumo wa nidhamu kuzingatia malezi, uwajibikaji, usalama na utu wa mtoto.
Sheria inaruhusu, lakini mjadala bado una nafasi ni muhimu kuanza kwa kuweka ukweli wazi. Tanzania Bara bado ina mfumo wa kisheria unaoruhusu adhabu ya viboko shuleni chini ya masharti maalumu.
Kanuni za Elimu za Adhabu ya Viboko za mwaka 2002 zinaweka utaratibu wa matumizi ya adhabu hiyo, ikiwamo kiwango kisichozidi viboko vinne kwa tukio.
Lakini kuwepo kwa sheria hakumaanishi kwamba mjadala kuhusu sheria hiyo umekwisha.
Sheria inaweza kuwa halali, lakini jamii bado inaweza kujiuliza kama inaendana na mahitaji ya wakati uliopo.
Ndiyo maana mjadala huu haupaswi kuishia katika swali la kama mwalimu amepiga viboko vinne au vitano.
Je, matumizi ya nguvu za mwili ni njia bora ya kujenga nidhamu kwa mtoto?
“Sisi tulipigwa na tukasoma”Hii ni hoja inayosikika mara kwa mara.Wapo wanaosema walipigwa shuleni na walifanikiwa katika maisha, hivyo hakuna tatizo kuendelea na mfumo huo.
Lakini ukweli kwamba mtu alipigwa na akafanikiwa hauwezi kuwa ushahidi kwamba kupigwa ndiko kulikomfanikisha.
Mafanikio ya mtu yanaweza kutokana na sababu nyingi, ikiwamo juhudi, mazingira ya familia, walimu, uwezo binafsi, fursa na elimu aliyopata.
Hivyo, hatuwezi kujenga sera ya taifa kwa kusema tu, “Sisi tulipigwa.”
Kila kizazi kina wajibu wa kujiuliza kama mbinu zilizotumika zamani bado ndizo bora kwa kizazi cha sasa.
Nidhamu si sawa na hofu,hapa ndipo tunapopaswa kutofautisha mambo mawili.
Nidhamu na hofu si kitu kimoja.Mwanafunzi anaweza kunyamaza kwa sababu anaogopa kupigwa, lakini hiyo haimaanishi ameelewa kwa nini anapaswa kuwa na nidhamu.
Anaweza kuacha kuchelewa kwa sababu anaogopa fimbo, lakini hilo si lazima limfundishe thamani ya muda.
Anaweza kuacha kufanya kosa kwa sababu anaogopa adhabu, lakini hilo halimaanishi amejifunza kuwajibika.
Nidhamu ya kweli ni pale mtoto anapofanya jambo sahihi kwa sababu anaelewa kuwa ni sahihi, si kwa sababu anaogopa kuumizwa.
Hapo ndipo mfumo wetu wa elimu unapaswa kuelekea.
Tatizo si walimu wote.
Mjadala huu usigeuke kuwa mashambulizi dhidi ya walimu. Walimu wana jukumu kubwa na gumu katika jamii. Wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto, wakisimamia wanafunzi wengi huku wakibeba majukumu ya kufundisha na kulea.
Tatizo kubwa ni mfumo,ikiwa tunataka kuondoa viboko, serikali lazima iwape walimu mbinu mbadala za kusimamia nidhamu.
Mwalimu afundishwe saikolojia ya mtoto, ushauri nasaha, usuluhishi wa migogoro na nidhamu chanya.
Hatuwezi kumwambia mwalimu asiitumie fimbo halafu tusimpe njia nyingine ya kushughulikia utovu wa nidhamu.
Mtoto anayekosea anahitaji kuwajibika,
kuondoa adhabu ya viboko hakumaanishi kuondoa nidhamu shuleni.Hili ni jambo ambalo serikali inapaswa kulisisitiza.
Mwanafunzi anayekiuka kanuni anapaswa kuwajibishwa.Lakini uwajibikaji unaweza kufanyika kwa njia nyingine.
Mwanafunzi anaweza kupewa onyo, ushauri nasaha, kuitwa kwa mzazi, kupewa mpango wa kurekebisha tabia au kuchukuliwa hatua nyingine za kinidhamu kulingana na ukubwa wa kosa.
Kwa mfano, mwanafunzi anayeharibu mali ya shule anaweza kuwajibishwa kwa kushirikishwa katika kurekebisha madhara aliyosababisha, kwa kuzingatia taratibu na uwezo wake.
Hapo mtoto anajifunza jambo muhimu: matendo yana madhara na kila mtu anapaswa kuwajibika.
Huo ni msingi bora wa malezi kuliko kumfanya mtoto aogope fimbo.
Tusubiri madhara ndipo tuchukue hatua?
Changamoto kubwa katika jamii yetu ni kwamba mara nyingi tunasubiri tatizo likue ndipo tunaanza kutafuta suluhisho.
Mwanafunzi akijeruhiwa baada ya kupigwa ndipo mjadala unaibuka.Familia inapolalamika ndipo viongozi wanaanza kuchunguza.Tukio linapokuwa kubwa ndipo jamii inaanza kuuliza kama mfumo una tatizo.
Hatuwezi kuendelea hivyo,kama tunajua mfumo unaweza kutumiwa vibaya na kusababisha madhara kwa mtoto, tunapaswa kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Kinga ni bora kuliko kusubiri mtoto kuumia ndipo tuchukue hatua.
Tanzania inataka kujenga kizazi gani?
Hili ndilo swali la msingi.Tanzania inataka mtoto anayemaliza shule awe mtu wa aina gani?
Tunataka awe mtiifu kwa sababu anaogopa mwenye mamlaka au tunataka awe mtu anayejua haki na wajibu wake, anayefikiri, anayejiamini na anayewajibika?
Leo tunazungumzia stadi za karne ya 21, ubunifu, teknolojia na uwezo wa mtoto kufikiri kwa kina.
Tunataka wanafunzi wawe na uwezo wa kuuliza maswali na kutatua matatizo.
Lakini mazingira ya kujifunzia nayo yanapaswa kwenda sambamba na malengo hayo.Mtoto anayejifunza kwa hofu si lazima awe mtoto anayejifunza kwa uelewa.
Serikali inaweza kuanza safari ya mabadiliko,kuondoa viboko hakupaswi kufanyika kwa kukurupuka.Serikali inaweza kuanzisha mchakato wa kitaifa wa mapitio ya mfumo wa nidhamu shuleni.
Walimu, wazazi, wanafunzi, wataalamu wa elimu, saikolojia, sheria na haki za mtoto washirikishwe.
Tafiti zifanyike,mifumo ya nidhamu mbadala itathminiwe,walimu wapewe mafunzo. na wazazi waelimishwe.
Na shule ziwe na mifumo ya wazi ya kushughulikia makosa ya wanafunzi.Baada ya hapo, sheria zinazohusu adhabu ya mwili zinaweza kufanyiwa marekebisho ili kuendana na mfumo mpya.
Tusichanganye huruma na kulegeza nidhamu,kuna wanaoweza kuhoji kuwa kuondoa viboko kutawafanya wanafunzi wawe wakaidi.
Hilo linaweza kutokea iwapo Serikali itaondoa fimbo bila kuweka mfumo mbadala.
Lakini ikiwa shule zitakuwa na kanuni zinazotekelezwa kwa uthabiti, wazazi wakishirikishwa na walimu wakapewa mafunzo, nidhamu inaweza kujengwa bila kutumia nguvu za mwili.
Kwa hiyo, hoja si kwamba mtoto asiadhibiwe.Hoja ni kwamba adhabu isimsaidie mtoto kuelewa kosa lake bila kuvunja utu wake.
Fimbo isiwe urithi wa lazima kila kizazi kina haki ya kuboresha kile kilichorithishwa. Kwamba mfumo fulani ulitumika zamani si sababu ya kuendelea nao milele.
Elimu yenyewe imebadilika,mitaala imebadilika,teknolojia imebadilika na mtazamo kuhusu malezi na haki za mtoto umebadilika.
Kwa nini nidhamu ibaki palepale?
Serikali haipaswi kuogopa kusema kuwa wakati umefika wa kubadili mfumo.
Huo si udhaifu ni utayari wa kujifunza na kuboresha Mtoto anahitaji nidhamu, lakini hahitaji lazima fimbo.Mwalimu anahitaji mamlaka ya kusimamia darasa, lakini mamlaka hiyo inaweza kutekelezwa bila kutumia nguvu za mwili.
Mzazi anahitaji mtoto mwenye nidhamu, lakini nidhamu inaweza kujengwa kwa ushirikiano kati ya familia na shule.
Tunachohitaji ni mfumo unaomfundisha mtoto kuwajibika, kuelewa makosa yake na kuheshimu sheria bila kumfanya aishi kwa hofu ya kupigwa.
Kwa hiyo, wakati umefika kwa Serikali kuanza mjadala wa mwisho kuhusu hatima ya adhabu ya viboko shuleni.
Tusubiri nini,mtoto mwingine kuumia, familia nyingine kulalamika au tukio kubwa zaidi kutokea?
Tanzania inahitaji kizazi kinachoheshimu sheria kwa uelewa, si kizazi kinachotii kwa hofu.
Fimbo inaweza kumfanya mtoto anyamaze, lakini elimu inapaswa kumfanya mtoto aelewe.
Na huo ndio wakati wa kuanza safari ya kuifanya fimbo kuwa historia katika shule zetu.
MWISHO.







0 Comments