Na Mwandishi wetu.
KATIKA Jitihada za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji mkoani Simiyu zimepata msukumo mpya baada ya vikundi vya wakulima vya vijana na wanawake kukabidhiwa pampu 120 za umwagiliaji zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800.
Ugawaji wa vifaa hivyo unalenga kuongeza tija, kubadilisha mfumo wa kilimo cha kutegemea mvua, na kuongeza kipato cha wakulima wadogo mkoani humo.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua zana za kisasa za kilimo cha umwagiliaji iliyofanyika wilayani Busega Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amewasihi wanufaika kuzitumia zana hizo kuongeza uzalishaji na kwa kulima kilimo chenye tija.
Macha amewataka wakulima hao kulinda pampu hizo kwa umakini mkubwa ili zilete manufaa endelevu, huku akitoa maelekezo kwa wataalamu wa kilimo mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima na kuwapa elimu stahiki ya kilimo cha kisasa.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Simiyu, Eng. Julius Lazaro amesema kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kuboresha na kujenga miundombinu mbalimbali ili kuwezesha wakulima kulima majira yote ya mwaka, na hivyo kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.
mwisho.







0 Comments