WAKULIMA WA PAMBA MASWA WAONYWA KUUZA KWA MKOPO.

 

Wakulima wa Pamba wakiuza Pamba yao kwenye ghala.

Na Samwel Mwanga, Maswa.

WAKULIMA  wa zao la pamba katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wametakiwa kutokubali kuuza zao hilo kwa mkopo na badala yake walipwe fedha zao mara moja wanapowasilisha pamba katika vituo vya ununuzi kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), ili kupunguza malalamiko ya kucheleweshwa kwa malipo.

Akizungumza leo, Agosti 11, 2026, katika kijiji cha Jilago wilayani humo Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Maswa, Lukas Kuwingwa, amesema mkulima anapaswa kulipwa fedha zake baada ya kukabidhi pamba yake kwa mnunuzi.

Kuwingwa ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wakulima wa kijiji hicho waliokabidhi pamba yao kwa ajili ya kuuzwa kwa Kampuni ya Alliance Ginner kupitia AMCOS ya Jilago, lakini hawakupata fedha zao kwa wakati.

Mkuu wa Takukuru wilaya ya Maswa,Lucas Kuwingwa akizungumza na wakulima wa zao katika kijiji cha Jilago wilayani humo. Picha na Samwel Mwanga

Amesema jumla ya Sh10 milioni zilihusika katika malipo ya wakulima 25, fedha ambazo zilihusishwa na pamba iliyokusanywa kwa bei ya Sh1,240 kwa kilo.

Kwa bei hiyo, Sh10 milioni ni sawa na takribani kilo 8,065 za pamba, ambazo wakulima walidai walikuwa hawajalipwa fedha zao baada ya kukabidhi zao hilo.

"TAKUKURU iliingilia kati suala hilo baada ya kupokea malalamiko ya wakulima na kuhakikisha hatua zinachukuliwa ili fedha zao zipatikane,"amesema.

Kwa upande wake, Afisa Ushirika Wilaya ya Maswa, Godfrey Mlanda, amewataka wakulima kutokabidhi pamba yao iwapo fedha za malipo hazipo katika kituo cha ununuzi.

“Uza pamba yako upate pesa yako, usikubali kukopwa. Ukikuta hakuna pesa kwenye kituo cha pamba, rudisha pamba yako nyumbani usubiri pesa iletwe,” amesema.

Baadhi ya wakulima wa zao la pamba wa kijiji cha Jilago wilaya ya Maswa waliojitokeza kwa ajili ya kulipwa fedha zao. Picha na Samwel Mwanga

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima, vyama vya ushirika na wanunuzi wa pamba, hasa inayotokana na kucheleweshwa kwa malipo.

Naye Katibu wa AMCOS ya Jilago, Khija Niga, amesema fedha hizo zilikopeshwa kwa wakulima kupitia bodi ya Jilago AMCOS, utaratibu huo ambao haukuwa sahihi.

Amesema hali hiyo ilisababisha wakulima 25 kudai jumla ya Sh10 milioni baada ya kukabidhi pamba yao lakini wamefanya jitihada kwa kushirikiana na TAKUKURU kuhakikisha kila mkulima analipwa pesa yake.

Baadhi ya wakulima waliopata fedha zao baada ya kuingiliwa kwa suala hilo na TAKUKURU wameishukuru Serikali kwa kuwasaidia kupata malipo yao.

Baadhi ya wakulima wa zao la pamba wa kijiji cha Jilago wilaya ya Maswa waliojitokeza kwa ajili ya kulipwa fedha zao. Picha na Samwel Mwanga

Yunice Emanuel amesema anashukuru hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia TAKUKURU, kwani aliweza kupata fedha zake baada ya kuwasilisha malalamiko kuhusu kutolipwa fedha za pamba aliyokuwa ameuza.

Naye Kwilasa Bundala amesema kupatikana kwa fedha hizo kumempa nafuu na kumsaidia kuondokana na changamoto iliyotokana na kucheleweshwa kwa malipo.

Kwa upande wake.Gulasa Masunga amesema ameishukuru serikali kwa hatua iliyochukuliwa kuhakikisha wakulima wanapata fedha zao.

"Hatua hiyo imetupa sisi wakulima matumaini kuwa malalamiko yetu yanaweza kusikilizwa na kufanyiwa kazi pale tunapokutana na changamoto katika uuzaji wa mazao "amesema.

Silya Ntemi amesema anashukuru TAKUKURU kwa kuingilia kati suala hilo na kusaidia wakulima kupata fedha zao baada ya kusubiri malipo.

Mkulima wa pamba, Ngusa Jitula (aliye kati) akipokea fedha kutoka kwa Katibu wa Jilago Amcos,Khija Niga (aliye kulia) mara baada ya kuuza pamba yake suala ambalo liliingiliwa na Takukuru.Picha na Samwel Mwanga.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa wakulima kwa kuwa fedha za pamba ni sehemu ya kipato wanachotegemea baada ya kutumia muda na gharama katika uzalishaji wa zao hilo.

Mwisho.








Post a Comment

0 Comments