MTOTO WA MIAKA MITANO AUAWA KIKATILI MASWA, WATEKAJI WATAKA SH. MILIONI 7.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Gulungwashi ambao walijitokeza kushuhudia mwili wa mtoto Samike Mponeja ambaye alitekwa na kisha kuuawa na mwili wake kukutwa juu ya mti.Picha na Samwel Mwanga


Na Samwel Mwanga, Maswa.

MTOTO wa kiume mwenye umri wa miaka mitano, Samike Mponeja, mkazi wa Kijiji cha Gulumwashi, Kata ya Malampaka wilayani Maswa, mkoani Simiyu, ameuawa kikatili baada ya kutekwa na watu wanaodaiwa kudai Sh7 milioni kutoka kwa wazazi wake.

Mwili wa mtoto huyo umepatikana leo, Agosti 19, 2026, ukiwa umetundikwa juu ya mti katika eneo la kichaka, siku 13 baada ya kutoweka alipokuwa akichunga ng’ombe.


Akizungumza katika eneo ambako mwili huo umepatikana, Suzanna Maduhu mkazi wa Malampaka amesema mtoto huyo alipotea Agosti 6, 2026 majira ya saa 7:00 mchana wakati akichunga ng’ombe akiwa pamoja na watoto wenzake watatu.


Amesema kabla ya kutoweka, mtoto huyo alikutwa na mmoja wa watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, ambaye alimtuma kwenda kuchukua fimbo katika eneo la kichaka, lakini hakurejea tena hadi mwili wake ulipopatikana leo.

“Mtoto alikuwa pamoja na wenzake watatu, ndipo mmoja wa watuhumiwa alipowakuta na kumtuma marehemu achukue fimbo eneo la kwenye kichaka, lakini hakurudi hadi leo tulipompata akiwa ameuawa,” amesema.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Gulumwashi, Mabala Shimbi amesema baada ya kupokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo, wananchi walianza juhudi za kumtafuta katika maeneo mbalimbali, lakini hawakufanikiwa kumpata.

Hata hivyo, amesema baadaye mmoja wa watu waliokamatwa akidaiwa kuhusika na tukio hilo alimpigia simu mama wa mtoto huyo na kumtaka kutoa Sh7 milioni, akidai mtoto wake ametekwa.

“Pamoja na kupiga simu, hao watekaji walimtumia huyo mzazi wa mtoto ujumbe mfupi wa maandishi wakimweleza kuwa ikifika saa 12:00 jioni hujatoa pesa hutaweza kumuona huyo mtoto. Na kweli tumempata mtoto akiwa ameuawa na kutundikwa juu ya mti,” amesema.

Polisi: Familia zisifiche wahalifu.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Chacha Maro, amesema Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.

Akiwa katika eneo ambako mwili wa mtoto huyo umepatikana, Maro amewataka wananchi kushirikiana na polisi katika kupambana na uhalifu, akisema mapambano hayo yanapaswa kuanzia ngazi ya familia.

Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu,Chacha Maro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Gulungwashi wilaya ya Maswa kufuatia kuuawa kwa mtoto,Samike Mponeja.Picha na Samwel Mwanga.

“Matatizo ya uhalifu hayaanzii mbali bali kwenye familia, hivyo kila familia ihakikishe haina mhalifu. Pamoja na kuwapa pole lakini nitoe elimu kwenu, tunao watuhumiwa watatu tunaendelea nao kwa hatua zaidi. Kwa sasa ipo haja kwa wananchi ya kushirikiana na Jeshi la Polisi, pingeni vitendo vya uhalifu kuanzia ngazi ya jamii,” amesema.

Maro amewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, huku akiwaonya dhidi ya kuchukua sheria mkononi kwa kwenda kuwaadhibu wazazi au ndugu wa vijana wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

DC Maswa: Watuhumiwa watafikishwa kwenye sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili wahusika wote wabainike na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akizungumza kufuatia tukio la mtoto,Samike Mponeja wa kijiji cha Gulungwashi kutekwa na kisha kuuawa.Picha na Samwel Mwanga

Amesema jamii inapaswa kujishughulisha na shughuli za uzalishaji zitakazowawezesha kupata kipato halali badala ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

“Wazazi niwaombe tusiwaachie watoto wadogo kuchunga mifugo mbali na maeneo ya nyumbani na niwahakikishie hakuna mtu yeyote aliyehusika katika tukio hili ataachwa salama. Tunaomba ushirikiano wenu ili kuhakikisha wahalifu wote wanapatikana ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini viashiria vya uhalifu katika jamii, ili matukio kama hayo yasijirudie wilayani humo.

Kifo cha Samike kimezua simanzi katika Kijiji cha Gulumwashi, huku wananchi wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi na hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa.

Mwisho.

Hiyo ni sehemu ambayo mwili wa mtoto,Samike Mponeja ulipokutwa juu ya mti akiwa ameuawa.Picha na Samwel Mwanga


Post a Comment

0 Comments