Askari wa jeshi la polisi wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya hospitali ya wilaya ya Maswa.Picha na Samwel MwangaNa Samwel Mwanga, Maswa.
JESHI la Polisi wilayani Maswa mkoani Simiyu limeadhimisha miaka 20 ya dhana ya Polisi Jamii kwa kufanya ya huruma ikiwemo kutembelea hospitali ya Wilaya ya Maswa, ambako kufanya usafi wa mazingira, kuchangia damu na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa.
Msaada huo umetolewa kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi za watoto na akinamama waliojifungua, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Jeshi la Polisi za kuimarisha uhusiano na jamii na kuonyesha kuwa askari ni sehemu ya wananchi wanaowahudumia.
Akizungumza Agosti 19, 2026 wakati wa shughuli hiyo, Mrakibu wa Polisi (SP) Ramadhani Mkimbu ambaye pia Mkuu wa kituo cha Polisi wilayani humo amesema maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii yamewapa fursa ya kwenda moja kwa moja kwa wananchi na kushiriki shughuli zenye manufaa kwa jamii.
Amesema kwa wilaya ya Maswa wameamua kuifikia hospitali hiyo kwa kufanya usafi, kuchangia damu na kutoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii.
“Hivi vitu vyote ambavyo tumevileta kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa katika wodi hizi za wazazi na watoto ni michango ya kila askari mmoja mmoja kutoka katika mfuko wake na hii ndiyo inayodhihirisha dhana hii ya Polisi Jamii,” amesema.
Mkimbu amesema askari polisi hawapaswi kuonekana kama maadui wa wananchi kwa kuwa nao ni sehemu ya jamii na wanatoka katika jamii hizo, hivyo ushirikiano kati yao na wananchi ni muhimu katika kukabiliana na uhalifu.
“Askari polisi ni sehemu ya jamii na si maadui kwa raia kwani wametoka katika jamii. Ni vizuri tukashirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali, zikiwemo za kupambana na uhalifu na wahalifu katika jamii,” alisema.
Amesema kazi za Jeshi la Polisi haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki, amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kufika hospitalini hapo na kushiriki shughuli za kijamii kimeonyesha wazi namna jeshi hilo lilivyo karibu na wananchi.
Amesema hospitali hiyo ina wagonjwa ambao uwezo wao wa kujihudumia ni mdogo, hivyo misaada iliyotolewa na polisi itawasaidia katika kipindi ambacho wanaendelea na matibabu.
“Tuna wagonjwa waliolazwa katika hospitali yetu ya wilaya ambao uwezo wao ni mdogo katika kujihudumia, hivyo kwa misaada hii itawasaidia. Hii pia imetufundisha hata sisi wenyewe kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wengine,” amesema.
Askari Polisi, Sajenti Anande Masay (kushoto) akitoa msaada kwa mmoja ya wagonjwa katika wodi ya Wazazi katika hospitali ya wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.Beatrice Julius, ambaye mtoto wake amelazwa katika hospitali hiyo akiendelea kupatiwa matibabu, aliishukuru jeshi hilo kwa msaada huo, amesema umeonyesha kuwa jeshi hilo linaweza kushirikiana na wananchi katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Alizitaka taasisi nyingine za Serikali na binafsi kuiga mfano huo kwa kutembelea wagonjwa na kusaidia hospitali katika maeneo mbalimbali kulingana na uwezo wao.
“Tunawashukuru polisi kwa kutukumbuka wakati huu ambao watoto wetu wako hospitalini. Tunaiomba taasisi nyingine nazo ziige mfano huu kwa sababu wagonjwa wanahitaji msaada na faraja kutoka kwa jamii,” amesema.
Naye Magreth Kadomola, aliyejifungua mtoto na kulazwa katika wodi ya wazazi, amesema kutembelewa na polisi pamoja na kupatiwa mahitaji mbalimbali kumempa hisia ya kuwa jeshi hilo lipo karibu na wananchi.
Amesema matukio kama hayo yanaweza kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama.
“Tunapowaona polisi wakija hospitalini kututembelea na kutusaidia, tunajisikia kuwa wako pamoja nasi. Hii inaongeza imani na ukaribu kati ya wananchi na polisi,” amesema.
Mkazi mwingine wa Maswa, Juma Ally, amesema ushiriki wa polisi katika shughuli za kijamii ni muhimu kwa sababu unawapa wananchi nafasi ya kuwaona askari nje ya mazingira ya utekelezaji wa majukumu ya kiusalama.
“Mara nyingi tunakutana na polisi wakati kuna tatizo au suala la usalama, lakini wanapokuja katika shughuli za kijamii tunajenga urafiki na kuondoa hofu. Hii inafanya hata mwananchi awe tayari kutoa taarifa anapoona uhalifu,” amesema.
Miongoni mwa vitu vilivyotolewa na askari hao ni sabuni za kufulia, mafuta ya kujipaka, pampasi za watoto, dawa za meno, maji na juisi, huku baadhi ya askari wakishiriki pia katika uchangiaji wa damu.
Shughuli hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya dhana ya Polisi Jamii, ambayo imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kupambana na uhalifu na kujenga jamii salama.
Mwisho.
Mrakibu wa polisi, Ramadhani Mkimbu akizungumza leo walipofika hospitali ya wilaya ya Maswa kutoa misaada kwa wagonjwa na kufanya usafi.Picha na Samwel Mwanga.





0 Comments