Na Costantine Mathias, Bariadi.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew ameonekana kukerwa na changamoto ya Usafi na ukusanyaji taka katika Mji wa Bariadi hasa maeneo ya sokoni pamoja na Usafi mitaro ya barabara kuzunguka Mitaa ya Mji huo ambao ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza kwenye Mkutano uliofanyika nyuma ya soko la jioni kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Kata ya Malambo, Mbunge huyo ameitaka Halmashauri hiyo kuwezesha vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 pamoja na kutekeleza miradi midogomidogo ikiwemo kupewa tenda za kufanya Usafi ili waweze kurejesha mikopo yao kwa wakati.
Mhandisi Kundo ambaye ameonyeshwa kusikitishwa na Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutumia mkandarasi kutoka Arusha ambaye amekuwa akikwamisha zoezi la ukusanyaji na uzoaji taka kutokana na uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari ya kuzoa taka.
"Suala la kukusanya taka Bado ni changamoto kwenye Mji wa Bariadi, tenda hizi zitolewe kwa makundi maalumu, tuwezeshe vijana na akina mama mitaji kupitia mikopo ya serikali ili waweze kujiajiri...Taka ni fursa, tuwape vijana fursa ya kukusanya Usafi ili Mazingita yawe safi, siyo lazima tupate mtu kutoka Arusha" amesema Mhandisi Kundo.
Nasibu Manywele kutoka kitengo cha Kudhibiti Taka Halmashauri ya Mji wa Bariadi, amesema kuwa kazi ya kuzoa taka katika Mji huo amepewa Mkandarasi kutoka Arusha ambaye magari yake matatu yatawasili jamatatu August 3, 2026 ili kuongeza jitihada katika ukusanyaji na uzoaji taka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Nkenyenge Charles amekiri kuwepo kwa changamoto ya Usafi katika Mji wa Bariadi huku akieleza kwamba Mji wa Bariadi bado ni mchafu.
"Tukiri kweli Mji wa Bariadi ni mchafu, tenda za uzoaji taka zinatangazwa kwa mfumo wa Nest na wanaoomba ni wadanganyifu...Kwa mfano, wanasema wana magari 40, Wafanyakazi 30 na vifaa lakini akipewa tenda haleti vifaa hivyo, mji wetu unakuwa kwa kasi na Robo hii tutaingiza kwenye vikao ili tushauriane namna nzuri ya kusafisha Mji wetu" ameeleza Nkenyenge.
Awali Vaileth Nyamikenda, mkazi wa Bariadi aliwasilisha kero ya Usafi hasa kuwepo kwa taka na uchafu katika soko la jioni ambalo limekithiri huku wananchi wakihofia mlipuko wa Magonjwa.
Mwisho.

0 Comments