Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
JULAI 9, 2026, Sakagoiblog, tulichapisha habari juu ya kijana Yoel Edward (30), akiomba msaada wa MATIBABU baada ya kujeruhiwa na mamba kwa kushambuliwa na Mamba miguu yote, hatimaye aumepata matibabu ya kukatwa miguu yote miwili.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Daktari kutoka kitengo cha Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Dkt. Edward Emanuel Mwasulama anasema kuwa mnamo Julai 13, 2026, walimpokea kijana aliyefahamika kwa jina la Yoel Edward akiwa na historia ya kushambuliwa na Mamba mwaka mmoja uliopita.
Anasema baada ya kumdadisi aliwaeleza kuwa alipatiwa Matibabu ya awali katila hospitali ya Morogoro na kuwekewa vyuma vya nje kwa muda wa mwaka mmoja na aliendelea na matibabu ya kusafisha vidonda lakini kwa bahati mbaya Vidonda havikushika.
Daktari kutoka kitengo cha Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Dkt. Edward Emanuel Mwasulama akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu matibabu ya Yoel Edward."Alipofika hapa vindonda vilikuwa vinatoa usaha mwingi na kuna baadhi ya sehemu ya mifupa ya miguu yote miwili ilikuwa tayari unapotea, baada ya mashauriano ya madaktari na madaktari Bingwa wa upasuaji wa Mifupa na mgonjwa mwenyewe tukaafikiana kwa pamoja kwamba matibabu ambayo yangemfaa mgonjwa kwa hali aliyokuwa nayo kulikuwa na sababu ya kukata mguu na bahati nzuri Yoel alipata udhamini wa huduma hiyo." amesema.
Kwa upande wake kijana Yoeli anasema kuwa alipatwa na tatizo la kushambuliwa na Mamba akiwa katika shughuli za kilimo, katika matibabu ya awali alikosa fedha za kuendelea na matibabu, hivyo kutokana na jitihada mbalimbali anawashukuru waaandishi wa Habari ambao walimtangaza na hatimaye Watanzania walimsaidia kwa kiwango kikubwa.
"Kweli waliguswa kwa kiwango kikubwa, na leo nimefikia hatua hii.. nilikuwa nimekata tamaa sababu miguu ilikuwa mibovu sana, maumivu yalikuwa makali na nilikuwa silali sababu ya maumivu, mpaka sasa kuna afadhali kidogo, baada ya kufika hapa hofu ilikuja sababu niliambia nitakatwa miguu kwani unapopewa taarifa ya kuondolea viungo (miguu) unapata hofu, nami nilipata hofu na baadae nilikubaliana na hali" anasema.
Anaeleza kuwa changamoto kuwa katika familia yao ilikuwa ni ukosefu wa fedha hali iliyomfanya kukata tamaa na pia chakula kulikuwa hakipiti, huku aliendelea kuwashukuru sana Watanzania na vyombo vya habari.
"Naomba pia wanisaidie kupata miguu ya Bandia ili kuendeleza ndoto ya kufanya Biashara ili kujimudu kimaisha tofauti na kushinda umekaa kwenye kitimwendo, kushumbuliwa na Mamba kumwekwamisha shughuli za kilimo na Biashara ya mpunga huko Morogoro, nikipata miguu ya bandia inaweza kunisaidia kuendeleza shughuli za Biashara kwa sababu sasa siwezi kufanya shughuli za kilimo" anasema na kuongeza.
"Ninamshukuru Mganga Mfawidhi wa Hospital hii kwa Usimamizi wa matibabu pamoja Madaktari wengine waliosimamia matibabu yangu...Navishukuru vyombo vya habari na Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu kwa kuniibua Watanzania wakanifahamu na kunisaidia matibabu".
Kwa upande wake mama Mzazi wa Yoel, Felister Nkinda Magembe, anasema " ninafurahi mwanangu kufanyia operation ya miguu na kupatiwa tiba, nawashukuru vyombo vya habari pamoja Watanzania kwa kumchangia fedha za Matibabu, nilihangaika sana na kufikia hali ya kuwa ombaomba kupitia Barua ya Mkuu wa Wilaya, kupitia vyombo vya habari tumepata fedha za matibabu ya kijana wangu".
Mwisho.










0 Comments