Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (wa pili kulia) akizungumza alipotembelea vipando vilivyopandwa katika eneo la shamba darasa la Jeshi la Magereza katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.
Samwel Mwanga, Bariadi
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, ametoa wito kwa washiriki wa maonesho ya kilimo ya Nanenane kanda ya mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi, mkoani Simiyu, kuhakikisha maonesho hayo yanatumika kutoa elimu itakayowasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kuongeza tija na kipato.
Akizungumza Agosti 2, 2026, alipotembelea mabanda na mashamba darasa ya taasisi mbalimbali amesema maonesho hayo yanapaswa kuwa darasa la vitendo litakalowawezesha wadau wa sekta ya kilimo kujifunza teknolojia mpya, mbinu bora za uzalishaji na namna ya kuongeza thamani ya mazao yao.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (kulia) akiagana na Kamishina Msaidizi wa Magereza, Hilary Kimbi(kushoto) mara baada ya kutembelea banda la maonesho la Magereza katika viwanja vya Nyakabindi. Picha na Samwel MwangaAmesema maonesho hayo ya Kanda ya Ziwa Mashariki yanayohusisha mikoa ya Simiyu,Shinyanga na Simiyu yatumike kuwabadilisha wananchi ili waweze kufanya shughuli zao kwa kuongeza tija katika uzalishaji hususani za kilimo,ufugaji na uvuvi kwa tija
"Ni muhimu wakulima watumie fursa ya maonesho haya kujifunza kanuni bora za kilimo. Mkulima wa mazao ya bustani anapaswa kufuata mbinu sahihi za uzalishaji ili kupata mazao yenye ubora na mavuno mengi. Sambamba na hilo, ni wakati wa kuwekeza zaidi katika kilimo cha biashara chenye tija na faida," amesema.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya mbegu bora, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkulima wa mbogamboga kutoka wilayani Bariadi, John Mwita, amesema maonesho hayo yamemsaidia kujifunza matumizi sahihi ya mbolea, umwagiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mazao.
Mmoja ya ng'ombe dume mwenye uzito wa kilogram 1050 akiwa kwenye banda la halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi. Picha na Samwel Mwanga." Nimeona teknolojia nyingi ambazo sikuwahi kuzifahamu. Elimu hii itatusaidia kuongeza uzalishaji na kupata mazao yenye ubora zaidi," amesema.
Naye Maria Nyamhanga, mkulima kutoka wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, amesema amevutiwa na mbegu bora za mazao ya bustani pamoja na elimu ya kuongeza thamani ya mazao baada ya kuvuna.
"Tunaomba maonesho kama haya yaendelee kila mwaka kwa sababu yanatupa nafasi ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu na taasisi mbalimbali," amesema..
Kwa upande wake, mfugaji kutoka Meatu mkoani Simiyu, Paulo Nyasi amesema amepata elimu kuhusu ufugaji bora, lishe ya mifugo na mbinu za kudhibiti magonjwa, akieleza kuwa maarifa hayo yatasaidia kuongeza uzalishaji wa mifugo na mapato ya wafugaji.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki mwaka huu yamewakutanisha taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali wa kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuonesha teknolojia, bidhaa na huduma zinazolenga kuongeza tija katika sekta hizo, ambazo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.
Mwisho.








0 Comments