ENG. KUNDO AJA NA SULUHISHO LA MAJI JIMBONI KWAKE.

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi mjini, Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kushoto) akikabidhi pampu za Maji Kwa ajili ya kupunguza Uhaba wa Maji kata ya Isanga.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

‎MBUNGE wa Jimbo la Bariadi mjini, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inatekeleza Mkakati wa dharura wa kupunguza tatizo la Maji safi na salama kwa kugawa pampu za maji kwa Wananchi wa Jimbo hilo.

‎Amesema kuwa kupitia Mkakati huo ambao umelenga kupunguza kero ya Maji kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya maji safi na salama, wakati wakisubiri suluhisho la Muda mrefu ambalo ni Mradi wa Maji wa Ziwa Viktoria ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 70.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew.

Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye ziara yake aliyoifanya katika Kata za Isanga, Nyangokolwa, Nyakabindi na Bunamhala, Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, alisema hawezi kuwaacha wananchi wakakosa Maji wakati kuna suluhisho la Muda mfupi.

‎Alisema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto za wananchi ikiwemo suala la upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.

‎Akiwa katika Kata ya Nyangokolwa, Mbunge huyo alikabidhi pampu 18 za maji ambazo zitafungwa kwenye visima ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama.

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi mjini, Mhandisi Kundo Mathew (katikati) akikabidhi pampu za Maji Kwa ajili ya kupunguza Uhaba wa Maji kata ya Nyakabindi.

‎"Tumekuja kutatua changamoto na matatizo ya wananchi, tutaweka uwazi, bayana juu ya Utekelezaji wa mipango ya serikali, tunataka kujua Mbunge wenu amewateteaje akiwa Bungeni...tumekuja kushukuru kwa kutupa kazi" alisema.

‎Akiwa kata ya Isanga, Mhandisi Kundo alikabidhi pampu za maji 17 ambazo zitafungwa kwenye visima vya Maji ili kuboresha upatikanaji wa Maji safi na salama kupitia Mpango wa dharura.‎

‎Nako kata ya Nyakabindi, Mhandisi Kundo alikabidhi Pampu 18 za maji huku akiwasisitiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Baruwasa) pamoja na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) kuhakikisha wanafunga pampu hizo kwenye visima walivyochimba wananchi ili waweze kupata Maji safi na salama.

‎Katika kata ya Bunamhala, Mhandisi Kundo amekabidhi pampu za maji 18 ili kuwapatia wananchi suluhisho la kupata huduma za Maji, huku akiwasisitiza wananchi kuwa hakuna kuchangia gharama za matengenezo ya pampu hizo.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Baruwasa), Mhandisi Nhandi Mathias alisema watahakikisha wanafanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri wa Maji ili wananchi wapate maji haraka kadri itakavyowezekana.

‎Katika mikutano yake Mhandisi Kundo, wananchi mbalimbali walijitokeza kuwasilisha changamoto ya Uhaba wa Maji katika maeneo yao na kuomba serikali kuwafikishia huduma za haraka na dharura ili waondokane na adha ya kutembea umbali mrefu kusaka huduma ya Maji.

‎Limi Silanga, mkazi wa Isanga aliiomba serikali kuwatatulia adha ya ukosefu wa Maji katika maeneo ambayo hawajafikiwa na huduma za maji.

‎Mwisho.















Post a Comment

0 Comments