SERIKALI YATOA SHILINGI MIL. 101 KUKARABATI VYUMBA VYA MADARASA BUPANDAGILA S/M. ‎

 

Jengo la Shule ya Msingi Bupandagila.

‎Na Costantine Mathias.

‎SERIKALI imetoa kiasi cha shilingi Mil. 101 kwa ajili ya Ukarabati wa Vyumba viwili vya madarasa na Ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Bupandagila,  ambayo imechakaa na kuanza kuhatarisha usalama wa wanafunzi wanaosoma Shuleni hapo.

‎Awali, Wakizungumza jana kwenye Mkutano wa Hadhara wakati wa kuwasilisha kero, wananchi hao walisema kuwa wanafunzi wa shule ya Msingi Bupandagila wapo hatarini kutokana na Vyumba vya madarasa kuwa nyufa zinazohatarisha usalama wa wanafunzi hao.


Jengo la Shule ya Msingi Bupandagila.

‎Joseph Mbogo mkazi wa Gisadi, alisema kuwa madasara hayo yalijengwa Kwa udongo saruji, na baada ya muda yalianza kuchakaa na kuhatarisha maisha watoto shuleni.

‎"Tunaomba serikali ifanye ukarabati wa mapema katika majengo hayo yasilete madhara...tumeambiwa serikali imeshatoa fedha, hivyo wafanye haraka kujenga madarasa hayo kwani majengo ya awali yalijengwa chini ya ubora na tunaomba yajengwe majengo ya Kisasa" alisema.

‎Makoye Kuleng'wa, mkazi wa Bupandagila alisema kuwa shule ya msingi Bupandagila matofali yaliyojengewa katika shule hiyo ni ya udongo na kufanya matofali hayo kushindwa kuhimili na kusababisha jengo kubomoka.

‎"Tunaishukuru serikali kwa kutoa fedha ili kukarabati majengo hayo waanze ujenzi haraka ili kunuusuru wananchi, madarasa hayo ni hatari sana Kwa wanafunzi wanaosoma hapo."

‎Akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara, Mbunge wa Jimbo la Bariadi mjini Mhandisi Kundo Mathew ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji alisema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa fedha kiasi cha shilingi Mil. 101 ili kukarabati majengo hayo ambayo amechakaa.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi mjini Mhandisi Kundo Mathew akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika kijiji cha Bupandagila.

‎Katika hatua nyingine, Mbunge huyo aliziomba Mamlaka za serikali ikiwemo Baruwasa na Ruwasa kuzifikishia huduma za maji sekta za Elimu (Shule) pamoja na Afya (zahanati) ili kurahisisha utoaji wa huduma.

‎"Pamoja na kupata fedha za kujenga Madarasa, lakini naomba mfikishe huduma za Maji mashuleni na kwenye vituo vya Afya pamoja na Umeme ili kurahisisha utoaji wa huduma." alisema Mhandisi Kundo.

‎Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Msingi ambaye ni Afisa Elimu maalum, Rutherford Magayane alisema kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi mil.101, Kwa ajili ya kukarabati Vyumba vya madarasa shuleni hapo.

‎Alisema kuwa tayari fedha hizo zimeshawekwa kwenye akaunti ya shule la serikali na kwamba wanasubiri maelekezo ili Ukarabati wa madasara hayo uanze rasmi.


‎Katika hatua nyingine Mbunge huyo alikabidhi mabati 250, mifuko ya saruji 250 Kwa ajili ya ukamilishani wa ofisi za mitaa pamoja na Pampu na mabomba yake 18 kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma ya Maji.

‎Mwisho.







Post a Comment

0 Comments