SERIKALI YAKABIDHI MTAMBO WA KISASA WA ZIMAMOTO NA UOKOAJI BUSEGA.

GARI la Zimamoto na Uokoaji lililokabidhiwa Leo wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.

SERIKALI imekabidhi Mtambo wa kisasa wa Zimamoto na Uokoaji katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, hatua inayolenga kuimarisha huduma za kukabiliana na majanga ya moto, kuokoa maisha ya wananchi na kulinda mali zao.

Akizungumza leo Juni 18, 2016, wakati wa hafla ya makabidhiano, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu, amesema mtambo huo utaongeza uwezo wa jeshi hilo kutoa huduma za dharura kwa haraka na ufanisi zaidi pindi majanga yanapotokea.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu.

Amesema mtambo huo utasaidia kuhudumia maeneo mbalimbali ya makazi, taasisi za umma pamoja na maeneo ya biashara ambayo yamekuwa yakihitaji huduma za zimamoto kwa wakati.

Kamanda Mtitu amefafanua kuwa mtambo huo una uwezo mkubwa wa kuhifadhi maji kwa ajili ya shughuli za kuzima moto na umewekewa vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha operesheni za uokoaji katika mazingira mbalimbali ya dharura.

Aidha, amesema kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linakuwa na vifaa vya kisasa vinavyoweza kukabiliana na changamoto za majanga yanayojitokeza katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faiza Salum, amesema ujio wa mtambo huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha usalama wa wananchi kwa kuimarisha huduma za dharura nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faiza Salum akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi gari za Zimamoto.

Amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Busega kuhakikisha mtambo huo unatunzwa na kutumika kwa ufanisi ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Hamidu Hamisi, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo mkubwa akieleza kuwa mtambo huo utasaidia kupunguza hasara zinazotokana na majanga ya moto pamoja na kuimarisha usalama wa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Hamidu Hamisi.

Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo walieleza kufurahishwa na hatua ya Serikali kupeleka huduma hiyo muhimu karibu nao, wakisema itarahisisha upatikanaji wa huduma za zimamoto na uokoaji kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza kwa niaba yao, Kulwa Ngololo mkazi wa Nyashimo, ameema awali walilazimika kutegemea huduma kutoka Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, hali iliyokuwa ikisababisha ucheleweshaji wa huduma wakati wa majanga.

Amesema mtambo huo unatarajiwa kuanza kutumika mara moja kuhudumia wananchi wa Busega na maeneo jirani, hatua itakayoongeza ufanisi wa huduma za dharura na kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya moto.

Mwisho.








Post a Comment

0 Comments