Na Mwandishi wetu, Dutwa-Bariadi.
SHIRIKA linalojihusisha na masuala ya kiuhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti leo Juni 18, 2026 wameikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi vifaa vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na vifaa vya kujikinga vyenye thamani ya shilingi 22,260,000 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori uitwao “Human-Wildlife Coexistence project”.
Akifafanua wakati wa makabidhiano hayo Meneja wa Operesheni wa Uhifadhi na Jamii Ndg. Christopher Christopher ameeleza kuwa vifaa vilivyokabidhiwa ni Pamoja na Fataki 90, Vilipuzi 29, Tochi zenye mwanga mkali 13, Vifanyio (balloons) 10, Unga wa pilipili Kilogramu 30, makoti ya mvua 15, Buti za mvua 15, Viatu vya usalama 15, Mabegi ya mkono 15 pamoja na Miwani za usalama 15.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Ndg. Halidi Mbwana amewashukuru wadau hao kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitaongeza ufanisi, usalama na mwitikio wa haraka kwa timu za kudhibiti Wanyama wakali na waharibifu zilizopo katika maeneo yanayopakana na hifadhi.
Mradi wa HWC uliozinduliwa rasmi tarehe 12 Agosti 2024 ukiwa na lengo la kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori ambapo hadi sasa mradi huu umefanikiwa kudhibiti Wanyama wakali na waharibifu kuingia katika makazi ya watu jambo ambalo linaimarisha ustawi wa jamii zinazozunguka hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na mapori ya akiba ya Maswa na Kijereshi.
Mwisho.
![]() |
![]() |






0 Comments