SAKATA LA DAKTARI KUMPIGA MUUGUZI HOSPITALI YA SOMANDA, LAMALIZWA KWA MARIDHIANO.

Baada ya maridhiano wajumbe wa kikao hicho walipeana mikono. Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga, Bariadi.

SAKATA lililotikisa Hospitali ya  Somanda iliyopo Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu, ambapo daktari alidaiwa kumpiga muuguzi wakiwa kazini, limefikia tamati baada ya pande husika kukutana na kuombana msamaha mbele ya viongozi wa sekta ya afya na serikali za mitaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Iddy Ndabona, amesema mgogoro huo ulitatuliwa kwa njia ya mazungumzo baada ya kubainika kuwa ulitokana na sintofahamu iliyojitokeza wakati watumishi hao walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kumhudumia mama mjamzito aliyekuwa akiandaliwa kwa ajili ya kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji wa Bariadi,Iddy Ndabona akizungumzia muafaka katika sakata la daktari kumpiga muuguzi katika hospitali ya Somanda mjini Bariadi. Picha na Samwel Mwanga.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, kikao maalumu kilichowakutanisha daktari na muuguzi husika pamoja na viongozi wa Hospitali ya Somanda, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wawakilishi wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Simiyu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kilifanyika na kufanikisha maridhiano kati ya pande hizo mbili.

Ndabona amesema kuwa katika kikao hicho kila upande ulipata nafasi ya kueleza mtazamo wake kuhusu tukio hilo, huku wote wakikubaliana kuacha tofauti zao na kuendelea kushirikiana katika kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Alisisitiza kuwa mazingira ya kazi yanahitaji utulivu, heshima na ushirikiano ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Mei 26, 2026 majira ya saa 7:00 mchana ndani ya chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Somanda. Inadaiwa kuwa mabishano yalizuka kati ya Daktari Idd Hamad na muuguzi Holo Kija wakati wa maandalizi ya upasuaji wa mama mjamzito, kabla ya hali hiyo kudaiwa kugeuka vurugu na kusababisha taharuki miongoni mwa watumishi waliokuwapo eneo hilo.

Sakata hilo lilizua mjadala mkubwa miongoni mwa watumishi wa afya na wananchi, huku baadhi wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu mazingira yaliyopelekea tukio hilo kutokea.

 Hata hivyo, baada ya maridhiano yaliyofikiwa, viongozi wa afya wamewataka watumishi wote kuzingatia maadili ya taaluma zao na kutumia njia za mazungumzo kutatua migogoro inayoweza kujitokeza mahali pa kazi.

Viongozi hao wameeleza kuwa kipaumbele kikuu kinapaswa kuwa ustawi wa wagonjwa na ubora wa huduma za afya, wakisisitiza kuwa matukio yanayoweza kuathiri utoaji wa huduma hayatakiwi kurudiwa katika vituo vya afya vya mkoa huo.

Mwisho. 



Post a Comment

0 Comments