RAIS SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA UDAKTARI WA HESHIMA NCHINI URUSI.

Na mwandishi wetu. 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na RUDN University katika hafla iliyofanyika Moscow, Urusi, tarehe 4 Juni 2026.

Tuzo hiyo imetolewa kutokana na mchango wake mkubwa katika mageuzi ya sekta ya elimu nchini Tanzania, kuimarisha diplomasia ya kimataifa, pamoja na juhudi zake za kukuza hadhi ya Tanzania duniani, hususan katika sekta ya utalii na ushirikiano wa kimataifa.


Katika hafla hiyo, Rais Samia alipokelewa na viongozi wa chuo hicho akiwemo Mkuu wa Chuo, Profesa Oleg Yastrebov, ambaye alimkabidhi rasmi shahada hiyo ya heshima mbele ya wageni mbalimbali na jumuiya ya wanafunzi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akicheza ngoma na Wanafunzi Watanzania wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi- (RUDN University), Moscow nchini Urusi, tarehe 04 Juni, 2026.

Baada ya kutunukiwa, Rais Samia alishiriki pia katika matukio ya kitamaduni ambapo alicheza ngoma pamoja na wanafunzi Watanzania wanaosoma katika chuo hicho, hali iliyodhihirisha mshikamano na furaha kati ya Tanzania na jumuiya ya wanafunzi walioko Urusi.


Aidha, Rais Samia alihutubia viongozi wa chuo, wanafunzi, na wageni waalikwa, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kielimu na kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi, pamoja na nafasi ya vijana katika kuleta maendeleo endelevu.

Mwisho.








Post a Comment

0 Comments