Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imezindua rasmi filamu ya Kifurushi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuelimisha wananchi kuhusu hatari za kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu na kushiriki kwa namna yoyote katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuwa tishio kwa maendeleo ya taifa kutokana na athari zake kwa afya, uchumi na ustawi wa jamii.
Alisema uchunguzi wa mamlaka hiyo umebaini kuwa baadhi ya wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kuficha dawa za kulevya katika mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida, hali inayowafanya baadhi ya wananchi kujikuta wakikabiliwa na mkono wa sheria bila kufahamu.
"Filamu hii imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna mtu anavyoweza kuingia kwenye mtego wa wahalifu kwa kubeba kifurushi au mzigo usiofahamika. Tunataka wananchi watambue kuwa mzigo unaoonekana wa kawaida unaweza kubeba dawa za kulevya na kubadilisha maisha yao kwa namna hasi," alisema Lyimo.
Aliongeza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia operesheni, uchunguzi, tiba kwa waathirika na kampeni za elimu kwa umma.
Kwa upande wake, Mchungaji Richard Hananja alisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki katika kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya kurejea katika maisha ya kawaida badala ya kuwanyanyapaa.
"Waraibu wanahitaji kusaidiwa na kupewa nafasi ya kubadilika. Viongozi wa dini, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushiriki katika kuwaongoza na kuwatia matumaini," alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa LATRA, Halima Lutabi, alisema sekta ya usafiri ni miongoni mwa maeneo ambayo wahalifu wamekuwa wakiyatumia kusafirisha dawa za kulevya, jambo linalohatarisha usalama wa abiria na taswira ya sekta hiyo.
Alisema LATRA itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola na wadau wa usafirishaji kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazodhibiti matumizi ya vyombo vya usafiri katika shughuli haramu zinasimamiwa kikamilifu.
Kwa upande wa sekta binafsi, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Abdallah Kiongozi, alisema chama hicho kiko tayari kushirikiana na Serikali katika kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri wa umma.
"Tunapokea filamu hii kwa mikono miwili na tuko tayari kuisambaza kwa wanachama wetu ili kuongeza uelewa kuhusu hatari za dawa za kulevya," alisema.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alisema filamu ni nyenzo muhimu ya kuelimisha jamii na kuhamasisha mabadiliko ya kitabia, akieleza kuwa kazi hiyo itasaidia wananchi kutambua hatari za kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.
Filamu ya Kifurushi inatarajiwa kuoneshwa katika mabasi yanayofanya safari za mikoani kote nchini kupitia ushirikiano kati ya DCEA, LATRA na Bodi ya Filamu Tanzania.
Ujumbe mkuu wa filamu hiyo ni kuwataka wananchi kutokubali kubeba mizigo, vifurushi au bidhaa za watu wengine bila kufahamu kilichomo, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwahusisha na makosa ya jinai yenye madhara makubwa kwa maisha yao, familia na jamii kwa ujumla.




















































0 Comments