SHILINGI BIL. 2.1 KUTEKELEZA MRADI WA MAJI VIJIJI VYA MWABAYANDA, MWASITA-MASWA.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk. Vicent Naano (aliye kati) akishuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Mauwasa na Kampuni ya Zongii ya mjini Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mwabayanda-Mwasita.Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga, Maswa.

WANANCHI  wa vijiji vya Mwabayanda na Mwasita wilayani Maswa mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa maji wenye thamani ya Sh 2.1 bilioni uliosainiwa kati ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) na mkandarasi Kampuni ya Zongii Contractors  Ltd ya jijini Mwanza.

Mradi huo unalenga kupunguza changamoto  ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu, hususan wanawake na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.

Akizungumza  Mei 30,2025  katika kijiji cha Mwasita wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatumia vifaa imara na vyenye viwango ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kama serikali ilivyokusudia.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mwasita wakati hafla ya utiaji wa saini katika ya Mauwasa na Mkandarasi kampuni ya Zongii ya Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mwabayanda-Mwasita.Picha na Samwel Mwanga.

Amesema serikali haitavumilia vitendo vya wizi au ubadhirifu katika utekelezaji wa mradi huo na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika kuhujumu utekelezaji wake.

“Tunataka mradi huu uwe wa mfano kwa sababu wananchi wamekuwa wakisubiri huduma hii kwa muda mrefu. Hakikisheni mnatumia vifaa bora na kazi ifanyike kwa uaminifu mkubwa,” amesema.

Amesema kuwa atahakikisha kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya watasimamia utekelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa Poas Kilangi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji safi na salama maeneo ya vijijini na mijini.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano (aliye kati) akishuhudia utiaji qa saini wa mkataba kati ya Mauwasa na Kampuni ya Zongii ya mjini Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mwabayanda-Mwasita.Picha na Samwel Mwanga.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja kutawanufaisha zaidi ya wananchi 12,000 na utasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

"Mradi huu utahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji kwenye mnara wenye urefu wa mita 12,lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji,ulazaji wa wa bomba kwa umbali wa kilomita 12 pamoja na mabirika ya kunyweshea maji mifugo,"amesema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Zongii Contractors  Ltd,Elpidius Kasiga amesema kuwa watakamilisha mradi huo mapema kwa kipindi cha miezi sita licha ya mkataba kuwataka kumaliza kwa kipindi cha mwaka mmoja ili wananchi waweze kupata hudumanya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Poas Kilangi(kulia)na Mwakilishi wa kampunibya Zongii Contractors Ltd,Elpidius Kasiga(kushoto)wakionyesha mikataba waliyosaini kwa ajili ya mradi wa maji wa Mwabayanda-Mwasita wilayani Maswa.Picha na Samwel Mwanga

"Tunahitaji ushirikiano kwa wananchi kwa ajili ya kulinda vifaa na miundo mbinu ya maji tutakayojenga na ninahaidi kutoa kipaumbele ya  ajira kwa vijana na wanawake wa vijiji vya Mwabayanda na Mwasita wakati wa utekelezaji wa mradi huu,"amesema.

Mkazi wa kijiji cha Mwasita Agnes John amesema kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakitegemea maji ya kwenye mito na visima vya asili ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.

“Tumekuwa tukipata shida sana hasa kipindi cha kiangazi. Wanawake tulikuwa tunaamka usiku kwenda kutafuta maji mbali, lakini sasa tuna matumaini makubwa,” amesema.

Sehemu ya wananchi walijitokeza kushuhudia uwekaji wa saini  kati ya Mauwasa na Kampuni ya Zongii katika kijiji cha Mwasita wilaya ya Maswa kwa ajili ya ujenzi wa mradi qa maji wa Mwabayanda -Mwasita. Picha na Samwel Mwanga.

Kwa upande wake, Esther Pius wa kijiji cha Mwasita amesema ujio wa mradi huo utaongeza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijiji hivyo.

“Ukipata maji karibu hata shughuli za kilimo na biashara zinaenda vizuri. Huu mradi utatusaidia sana wananchi wa kawaida,” amesema.

Naye  Neema Masule mkazi wa kijiji cha Mwabayanda amesema watoto wengi walikuwa wakichelewa kwenda shule kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.

“Watoto wetu walikuwa wanateseka sana. Tunaamini sasa hali itabadilika na afya za wananchi zitakuwa bora zaidi,” amesema.

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments