Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akiongoza kikao cha kamati ya mazao ya wilaya hiyo kwa ajili ya ununuzi wa zao la pamba wilayani humo.Picha na Samwel MwangaNa Samwel Mwanga, Maswa.
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dkt Vicent Naano amewaonya viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (Amcos) wilayani humo kuacha mara moja tabia ya kuiba fedha za makampuni ya ununuzi wa zao la pamba katika msimu wa ununuzi wa mwaka 2026/2027.
Dkt. Naano ametoa onyo hilo wakati akizungumza katika kikao cha Kamati ya Mazao wilayani Maswa, ambapo amesema baadhi ya makatibu wa Amcos wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa kuiba fedha zinazotolewa na makampuni kwa ajili ya kuwalipa wakulima wa pamba.
Amesema serikali haitavumilia tena vitendo hivyo vinavyowaumiza wakulima pamoja na kudhoofisha uaminifu kati ya makampuni ya ununuzi na Amcos.
“Wapo baadhi ya makatibu wa Amcos ambao kila msimu malengo yao ni kuiba fedha za makampuni zilizoletwa kwa ajili ya kuwalipa wakulima. Hili hatutalivumilia tena,” amesema Dkt Naano.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo serikali haiwezi kuyafumbia macho ni viongozi kutumia nafasi zao vibaya kwa kuiba fedha za makampuni na kuwaumiza wakulima ambao hutegemea malipo hayo kwa shughuli zao za maisha.
Aidha amesema katika msimu uliopita tayari imebainika kuwepo kwa wizi mkubwa katika baadhi ya Amcos, huku baadhi ya vyama vikikusanya fedha nyingi lakini mwisho wa msimu kushindwa kuonyesha mapato halali au kubaki bila fedha.
Baadhi ya wadau wa sekta ya zao la pamba katika wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Mazao ya wilaya hiyo. Picha na Samwel MwangaKutokana na hali hiyo, amesema serikali ya wilaya imepanga kubadili mfumo wa utoaji wa fedha katika Amcos ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji wakati wa ununuzi wa zao hilo.
“Amcos kwa msimu mzima zinafanya kazi na zinakusanya fedha za ushuru kutoka kwa makampuni ya ununuzi wa pamba, lakini mwisho wa msimu wanadai hawana fedha. Kwa mwaka huu kila Amcos ihakikishe inakarabati maghala yanayotumika kununulia pamba kwani mengi yamechakaa wakati fedha wanapata,” amesema.
Pia amesisitiza kuwa viongozi wote wa Amcos waliobainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha katika msimu uliopita wanapaswa kuondolewa mara moja katika nyadhifa zao ili kupisha viongozi waaminifu.
Mbali na hilo, Dkt Naano ameyataka makampuni ya ununuzi wa pamba wilayani humo kuhakikisha yanarejesha faida kwa jamii kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kujikita katika biashara pekee.
Amesema makampuni hayo yanapaswa kuacha alama kwa wananchi kupitia miradi ya kijamii inayogusa maisha ya wananchi, hususan katika sekta za maji, elimu na afya.
Amelitaja SM Holding Ltd kuwa mfano wa kampuni iliyotekeleza wajibu wake kwa jamii baada ya kuchimba visima viwili vya maji katika vijiji vya Sangamwalugesha na Mwamitumai wilayani humo.
“Tunataka makampuni mengine yaige mfano huu wa kurejesha faida kwa jamii. Wananchi wanapaswa kuona matunda ya uwepo wa makampuni hayo katika maeneo yao,” amesema.
Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Cosmas Budodi amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa dhidi ya viongozi waliohusika na ubadhirifu huo.
Amesema viongozi wote wa Amcos waliobainika kuhusika na wizi wa fedha za wakulima katika msimu uliopita wameondolewa katika nafasi zao huku baadhi yao tayari wamefikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
“Hatutakuwa tayari kuona fedha za wakulima zinapotea kutokana na uzembe au ubadhirifu wa viongozi wachache. Sheria itachukua mkondo wake kwa wote waliohusika,” amesema.
Mkulima wa kijiji cha Ng’haya, Jumanne Jimoga amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao bila sababu za msingi huku fedha zikidaiwa kupotea kwenye usimamizi wa Amcos.
“Sisi tunateseka sana, unauza pamba lakini fedha zinachelewa au unapunjwa. Serikali isimamie kweli hawa viongozi,” amesema.
Naye Maria John, mkulima kutoka kijiji cha Buyubi amesema hatua ya Mkuu wa Wilaya kuwataka viongozi waliohusika na wizi kuondolewa itasaidia kurejesha imani kwa wakulima.
“Tunataka viongozi waaminifu watakaolinda fedha za wakulima. Pamba ndiyo tegemeo letu kubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Paulo Ndege wa kijiji cha Bugarama amesema mfumo mpya wa utoaji fedha ukisimamiwa vizuri unaweza kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza kila msimu wa mauzo ya pamba.
“Fedha zikisimamiwa vizuri wakulima watanufaika na kilimo chao badala ya watu wachache kujinufaisha,” amesema.
Mwisho.






0 Comments