Na Samwel Mwanga, Maswa.
FURAHA ya kupata watoto watatu mapacha kwa wakati mmoja imegeuka kuwa changamoto kwa Prisca James John, mkazi wa kijiji cha Budekwa wilayani Maswa mkoani Simiyu, baada ya kushindwa kumudu gharama za maziwa ya unga kwa watoto hao waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa.
Prisca ambaye amejifungua watoto watatu wa kike katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa amesema hali yake ya kiuchumi ni ngumu kiasi kwamba anashindwa kununua maziwa ya kuwasaidia watoto hao wanaohitaji uangalizi maalumu.
Watoto watatu waliozaliwa na Prisca James John, mkazi wa kijiji cha Budekwa wilayani Maswa mkoani Simiyu wakiwa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Maswa katika wodi ya watoto njiti.Picha na Samwel Mwanga.Akizungumza leo Mei 8,2026 akiwa katika wodi ya watoto njiti hospitalini hapo, Prisca amesema maziwa yake ya asili hayatoshi kuwanyonyesha watoto hao wote, hali inayomlazimu kutumia maziwa ya unga ambayo gharama yake ni kubwa kwake.
“Mie maziwa yangu yapo kidogo hayawatoshelezi hawa watoto, hivyo naomba nisaidiwe ili kuweza kupata maziwa ya unga. Kopo moja la maziwa linatumika kwa muda wa siku tatu au nne na ni gharama yaani kopo moja ni sawa na Sh 40,000/=, na mimi sina uwezo huo,” amesema Prisca kwa huzuni.
Muuguzi wa wodi ya watoto njiti hospitalini hapo, Tausi Buriki amesema watoto hao walizaliwa kwa njia ya kawaida wakiwa na umri wa miezi nane tumboni, hivyo wanahitaji uangalizi wa karibu pamoja na lishe maalumu ili kuendelea kuwa salama.
Amesema kutokana na hali ya mama huyo, bado kuna umuhimu wa wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wasamaria wema kujitokeza kusaidia mahitaji muhimu ya watoto hao ikiwemo maziwa ya unga na vifaa vya watoto.
Muuguzi Tausi Buriki (kushoto) wa wodi ya watoto njiti katika hospitali ya wilaya ya Maswa akizungumza na Prisca James John (kulia), mkazi wa kijiji cha Budekwa wilayani Maswa mkoani Simiyu aliyejifungua watoto watatu kwa njia ya kawaida. Picha na Samwel Mwanga“Watoto hawa ni njiti, wanahitaji uangalizi wa karibu na lishe ya kutosha. Mama mwenyewe hali yake siyo nzuri kiuchumi hivyo msaada unahitajika kwa haraka,” amesema Tausi.
Imeelezwa kuwa huu ni uzao wa pili kwa Prisca ambapo mtoto wake wa kwanza pia alizaliwa kwa njia ya kawaida.
Baadhi ya wananchi waliopata taarifa za tukio hilo wameanza kutoa wito kwa jamii, taasisi na viongozi kujitokeza kusaidia familia hiyo ili kuhakikisha watoto hao wanapata huduma zinazohitajika katika hatua za awali za maisha yao.
Mwisho.






0 Comments