TAMWA WAKUTANA DAR, WAJIFUNZA HAKI ZA WAFANYAKAZI NA MIKAKATI YA MAFANIKIO.


Na Mwandishi wetu.


WAFANYAKAZI wametakiwa kufuata na kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha anapata stahiki zake kwa haki na usahihi pindi wanapokumbana na changamoto akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikazi. 

Wito huo umetolewa na Mwakilishi kutoka Mfuko wa Taifa kwa Wafanyakazi Mahala pa Kazi (WCF), Kombo Hassan, wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika mkutano wao wa mwaka uliofanyika eneo la Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika semina iliyotangulia mkutano huo, Hassan alisema kuwa wafanyakazi wengi hukosa haki zao si kwa sababu ya kukosa sifa, bali kutokana na kutofahamu au kutofuata taratibu sahihi za kisheria na kiutendaji. 


Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wafanyakazi kutoa taarifa za changamoto wanazokutana nazo kwa wakati na kupitia njia rasmi ili ziweze kushughulikiwa ipasavyo.

“Ni muhimu kwa mfanyakazi kuelewa wajibu wake pamoja na haki zake. Anapopata changamoto kazini, asikimbilie njia zisizo rasmi, bali afuate utaratibu uliowekwa ili kupata suluhisho la kudumu,” alisema Hassan.

Aidha, alibainisha kuwa Mfuko wa WCF una jukumu la kulinda na kusimamia maslahi ya wafanyakazi wanapopatwa na madhara wakiwa kazini, ikiwa ni pamoja na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.


 Aliongeza kuwa mfuko huo unaendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi na waajiri ili kuhakikisha kila mmoja anatambua wajibu wake katika kulinda usalama na afya mahala pa kazi.

Kwa upande wao, baadhi ya wanachama wa TAMWA walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewasaidia kuelewa zaidi namna ya kushughulikia changamoto za kikazi kwa kufuata taratibu stahiki.


Walieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu hasa kwa wanahabari ambao mara nyingi hukutana na mazingira hatarishi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mkutano huo wa siku mbili wa TAMWA hufanyika kila mwaka na hutanguliwa na semina maalum ya kuwajengea uwezo wanachama wake.


Semina hiyo hulenga kuimarisha uelewa katika masuala mbalimbali ya habari, maendeleo ya jamii, pamoja na kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo, na mikakati ya baadaye ya chama hicho.

Mbali na hilo, mkutano huo pia hutoa fursa kwa wanachama kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za kazi, na kujadili masuala muhimu yanayogusa taaluma ya uandishi wa habari na ustawi wa jamii kwa ujumla. 


Pia ni jukwaa muhimu la kupokea wanachama wapya na kuimarisha mshikamano ndani ya chama hicho.

Kwa ujumla, washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza na kushirikiana ili kuboresha utendaji kazi wao na kuhakikisha wanachangia ipasavyo katika maendeleo ya jamii.

 Walisema kuwa kupitia majukwaa kama hayo, wanapata nafasi ya kujengeana uwezo na kuimarisha taaluma yao kwa manufaa ya taifa.

Mwisho.





Post a Comment

0 Comments